
Wataalamu wa magari wameeleza kuwa kuna utaratibu muhimu unaoshauriwa kufuatwa wakati wa kupaki gari aina ya automatic ili kulinda mfumo wa gia na kuongeza usalama.
Utaratibu huo huanza kwa dereva kuhakikisha gari limesimama kabisa akiwa amekanyaga breki. Kisha gia hutolewa kutoka kwenye “Drive (D)” kwenda “Neutral (N)” kabla ya kuvuta breki ya mkono (hand brake).
Baada ya kuvuta hand brake, dereva anatakiwa kuondoa mguu taratibu kwenye breki ili uzito wa gari ushikiliwe na breki ya mkono badala ya mfumo wa gia. Hatua hiyo husaidia kupunguza presha kwenye gia hasa gari linapokuwa limeegeshwa kwenye mteremko.

Kisha dereva hukanyaga tena breki na kuhamisha gia kwenda “Parking (P)” kabla ya kuzima injini. Wataalamu wanasema njia hiyo ni salama zaidi na inaweza kusaidia kuongeza uimara wa mfumo wa transmission ya gari.
Madereva wanashauriwa kuzoea utaratibu huo ili kuepuka uharibifu wa mapema wa gearbox pamoja na kuongeza usalama wa gari linapokuwa limeegeshwa.