
Rais wa Marekani, Donald Trump amesema Iran imeidungua moja ya Helikopta za kisasa za kijeshi za Marekani aina ya Apache wakati ikiwa katika doria kwenye eneo katika Mlango Bahari wa Hormuz usiku wa kuamkia leo.
Kupitia taarifa yake, Trump alisema marubani wawili waliokuwa ndani ya helicopta hiyo wako salama na hawakupata majeraha yoyote licha ya tukio hilo kubwa kutokea.
“Nimepata taarifa hivi punde kutoka kwa jeshi letu kubwa kwamba usiku uliopita Wairani waliidungua moja ya helikopta zetu za kisasa sana aina ya Apache wakati ilikuwa ikifanya doria katika eneo la Strait of Hormuz.”alisema Trump.

Hata hivyo, Trump ameonya kuwa Marekani italazimika kujibu shambulio hilo, akisema hatua hiyo haiwezi kupuuzwa kutokana na uzito wake kwa usalama wa taifa hilo.
Kauli hiyo imeongeza taharuki mpya kuhusu mvutano unaoendelea kati ya Marekani na Iran, huku wachambuzi wa siasa za kimataifa wakihofia tukio hilo linaweza kuongeza hali ya sintofahamu katika eneo la Mashariki ya Kati.
Mpaka sasa, Iran bado haijatoa taarifa rasmi kuhusu madai hayo yaliyotolewa na Rais Trump.
