
Mwamuzi wa kimataifa kutoka Somalia, Omar Abdulkadir Artan, ametangazwa rasmi na UEFA kuwa mwamuzi wa mchezo wa UEFA Super Cup 2026 utakaowakutanisha mabingwa wa Ulaya, Paris Saint-Germain (PSG), dhidi ya mabingwa wa Europa League, Aston Villa.
Mchezo huo wa kifahari unatarajiwa kuchezwa tarehe 12 Agosti katika jiji la Salzburg, Austria, ukiwakutanisha mabingwa wa mashindano makubwa mawili ya klabu barani Ulaya.
Uteuzi wa Artan unakuja siku chache baada ya kushindwa kushiriki Kombe la Dunia 2026 nchini Marekani kufuatia matatizo ya kuingia nchini humo, licha ya kuwa alikuwa miongoni mwa waamuzi walioteuliwa na FIFA.
UEFA na CAF zimesema uteuzi huo ni sehemu ya ushirikiano wao mpya wa kuendeleza waamuzi wa kiwango cha juu, huku Artan akitambuliwa kama mmoja wa waamuzi bora zaidi barani Afrika baada ya kutwaa tuzo ya Mwamuzi Bora wa Kiume wa Afrika mwaka 2025.
Kwa wengi nchini Somalia, uteuzi huu ni heshima kubwa na ushahidi wa mafanikio ya Artan katika soka la kimataifa, ambapo ameendelea kuweka historia kama mmoja wa waamuzi wanaoipa Somalia sifa katika jukwaa la dunia.