×

Serikali Yapendekeza Mgao Mpya wa Mapato ya Kodi ya Pango la Ardhi

Serikali imependekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Ardhi, Sura ya 113, kwa lengo la kuweka utaratibu mpya wa mgawanyo wa mapato yatokanayo na kodi ya pango la ardhi ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa sekta hiyo.

Akiwasilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar, amesema Serikali inapendekeza asilimia 20 ya mapato yanayokusanywa kutokana na kodi ya pango la ardhi irejeshwe kwa taasisi husika ili kuboresha huduma na usimamizi wa ardhi.

Kwa mujibu wa pendekezo hilo, asilimia 10 ya mapato hayo itaelekezwa kwa wizara yenye dhamana ya masuala ya ardhi, huku asilimia nyingine 10 ikipelekwa kwa mamlaka za serikali za mitaa.

Waziri Khamis amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi zinazoshughulikia masuala ya ardhi pamoja na kuongeza ufanisi katika shughuli za upimaji wa ardhi, utoaji wa hati na ukusanyaji wa kodi ya pango la ardhi.

Aidha, ameeleza kuwa utaratibu maalumu utaandaliwa na Wizara ya Fedha ili kuhakikisha fedha zitakazotolewa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuleta tija katika maendeleo ya sekta ya ardhi nchini.

Serikali inaamini kuwa marekebisho hayo yataongeza uwezo wa mamlaka husika kusimamia rasilimali za ardhi kwa ufanisi zaidi, sambamba na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Leave a Comment