
Mahakama Kuu, Masijala Ndogo Kanda ya Dar es Salaam, imewaachia huru watuhumiwa watatu waliokuwa wakikabiliwa na shtaka la mauaji ya Atuswege Anyagenye, maarufu kama Mama Emma, baada ya kubaini kuwa ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka haukutosha kuthibitisha tuhuma dhidi yao.
Watuhumiwa hao ni Zaburi Kitalamo, mfanyabiashara Roger Salum (25), maarufu kwa jina la Mayala, mkazi wa Utewe wilayani Urambo mkoani Tabora, pamoja na Furaha Ngamba (47), anayefahamika kama mganga wa kienyeji na mkazi wa Uyogo wilayani humo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, ilidaiwa kuwa Desemba 12, 2020, katika eneo la Kinzudi, wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam, watuhumiwa hao walimuua Atuswege Anyagenye ambaye alikuwa mke wa mtuhumiwa wa kwanza, Zaburi Kitalamo, na baadaye kuutupa mwili wake.
Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji David Ngunyale, ambaye alisema ushahidi uliowasilishwa mahakamani haukujitosheleza kuwaunganisha watuhumiwa hao na kosa lililokuwa likiwakabili, hivyo kuamuru waachiwe huru kwa mujibu wa sheria.