
Jeshi la Polisi mkoani Arusha linamshikilia mtu mmoja aitwaye Lameck Jonathan Mlay (30) mfanya usafi na mkazi wa Maji ya Chai kwa tuhuma za mauaji ya Husna Shabani (33) mkazi wa Majengo Jijini Arusha na kisha kutupa mwili huo katika chemba ya maji taka.
Akitoa taarifa hiyo leo Juni 15, 2026 Kamanda wa Polisi Mkoani humo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amesema mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Juni 14, 2026 muda wa jioni huko katika Bar iitwayo Shisha Village iliyopo kata Elerai Jijini Arusha.
Kamanda Masejo amebainisha kuwa mtuhumiwa alimjeruhi mhanga sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababisha umauti, kisha kwenda kuutupa mwili huo katika chemba ya maji taka iliyopo katika bar hiyo.
Ameendelea kufafanua kuwa uchunguzi wa awali wa Jeshi hilo umebaini kuwa kabla ya tukio hilo, mtuhumiwa na marehemu walikuwa pamoja kwenye starehe katika eneo hilo, huku akibainisha wanakamilisha uchunguzi kwa taratibu nyingine za kisheria.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuheshimu utu na uhai wa wengine, kwa kutatua migogoro kwa njia za amani na kutoa taarifa za uhalifu ili kuimarisha usalama na amani katika jamii.
