
Kundi la Hezbollah limetangaza kuwa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Marekani na Iran ya kumaliza mzozo wa Mashariki ya Kati yamechangia kufikiwa kwa usitishaji mpana wa mapigano unaojumuisha pia Lebanon.
Katika taarifa yake, Hezbollah ilisema kuingizwa kwa Lebanon katika hati ya makubaliano kati ya Washington na Tehran kunaonyesha dhamira ya Iran ya kumaliza vita na kuhakikisha mapigano yanakoma katika maeneo yote yaliyoathirika na mzozo huo.
Kundi hilo linaloungwa mkono na Iran limeonya kuwa halitakubali mashambulizi yoyote yatakayokiuka mamlaka ya Lebanon au kuhatarisha usalama wa wananchi wake. Aidha, limesisitiza kuwa Lebanon ina haki ya kujilinda na kulinda ardhi yake hadi pale ambapo vikosi vya Israel vitaondoka kikamilifu na wafungwa wa Lebanon kurejeshwa.
Hezbollah pia ilitoa shukrani kwa viongozi, jeshi na wananchi wa Iran kwa kile ilichokitaja kuwa msaada wao mkubwa kwa Lebanon, pamoja na kusisitiza umuhimu wa Lebanon kujumuishwa katika makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano.
Wakati huo huo, afisa mmoja wa Hezbollah amesema kundi hilo halijafanya operesheni yoyote ya kijeshi tangu kutangazwa kwa makubaliano ya Marekani na Iran. Afisa huyo, ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema msimamo wa Hezbollah kuhusu usitishaji mapigano unategemea namna Israel itakavyoheshimu makubaliano hayo.
Pia alidai kuwa Iran ilichelewesha kusaini makubaliano hayo na Marekani ili kufuatilia kwanza kama Israel ingeendelea kuheshimu usitishaji wa mapigano nchini Lebanon.