
MSIMAMIZI wa tanki Kassim Kongwa na wenzake, wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa shataka la wizi wa lita 2,800 za mafuta ya ghafi mali ya kampuni ya Mikoani Edible Oil and Detergents Limited.
Washtakiwa wengine ni Hemed Abdallah, Hassan Kimoge, Juma Issah, Halfan Halfan maarufu kama Ruba, Maria Gulaba ambao ni opereta wa kiwanda hicho na mlinzi Jafar Molel.
Washtakiwa hao wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Anna Magutu.
Akiwasomea mashtaka, wakili wa serikali Winiwa Kasala alidai, kati ya Juni 2 na 4, mwaka huu jijini Dar es Salaam,kwa nia ovu, washtakiwa hao waliongoza genge la uharifu na kuiba mafuta ghafi mali ya kampuni hiyo.

Winiwa alidai, Juni 4, mwaka huu mtaa wa Moringe, Wilaya ya Temeke, washtakiwa hao waliiba lita 2800 za mafuta ghafi ya thamani ya sh milioni 26, mali ya kampuni hiyo.
Wakili Winiwa pia amedai, washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la utakatishaji.Alidai, katika tarehe na eneo hilo washtakiwa hao walijipatia lita 2800 za mafuta wakijua mafuta hayo yalitokana na kksa tangulizi la wizi.
Baada ya kusomewa mashtaka washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwasababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi.
Upande wa jamhuri umedai, upelelezi haujakamilika hivyo kesi imeahirishwa hadi Juni 30,2026 itakapotajwa.
Washtakiwa wote wamepelekwa mahabusu kwasababu shtaka la utakatishaji fedha halina dhamana.