×

Iran Kupata Uwekezaji wa Trilioni 788 Baada ya Makubaliano na Marekani

Mfuko maalumu wa uwekezaji wa sekta binafsi wenye thamani ya dola bilioni 300 za Marekani (Sawa na Shilingi Trilioni 788.1 za Tanzania) unaolenga kuchochea uwekezaji nchini Iran umejumuishwa katika makubaliano ya mfumo kati ya Marekani na Iran, huku zaidi ya nusu ya fedha hizo tayari zikiwa zimeahidiwa na wawekezaji mbalimbali.

Kwa mujibu wa chanzo kilicho karibu na mazungumzo hayo, mfuko huo unakusudiwa kutoa motisha za kiuchumi kwa pande zote mbili ili kufanikisha makubaliano ya mwisho yatakayomaliza vita kati ya Marekani na Iran. Makubaliano hayo yanatarajiwa kutiwa saini rasmi siku ya Ijumaa Juni 19, 2026.

Mfuko huo, unaotarajiwa kuitwa Reconstruction and Development Fund, hautakuwa mpango wa fidia wala msaada wa serikali, bali utategemea fedha za sekta binafsi pekee. Kampuni kutoka Marekani, nchi za Ghuba ya Kiarabu, Asia, Amerika Kusini na Afrika zimeahidi kuchangia fedha kwa ajili ya uwekezaji katika sekta za nishati, usafirishaji, viwanda na miundombinu.

Iran awalidai fidia ya dola bilioni 400 kutoka Marekani kwa uharibifu uliosababishwa na vita, lakini Marekani ilikataa kutoa fedha hizo. Hapo ndipo wazo la kuanzisha mfuko huu wa uwekezaji lilipoibuka kama njia mbadala ya kusaidia kufufua uchumi na miundombinu ya Iran.

Fedha hizo zinatarajiwa kusaidia ukarabati wa maeneo yaliyoharibiwa na vita, ikiwemo viwanda vikubwa kama Mobarakeh Steel, viwanda vya kusafisha mafuta, viwanja vya ndege pamoja na miundombinu mingine muhimu.

Iran imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje kwa zaidi ya miongo minne kutokana na vikwazo vya Marekani na jumuiya ya kimataifa. Hata hivyo, taifa hilo lina utajiri mkubwa wa rasilimali za mafuta na gesi pamoja na idadi ya watu zaidi ya milioni 92 wenye elimu na nguvu kazi inayokua.

Leave a Comment