
Tanzania inaendelea kung’ara katika medani ya karate kimataifa kupitia Rumadha Fundi, mwenye Mkanda Mweusi Dan ya 6 na Mkufunzi Mkuu wa Tanzania Jundokan Karate-do, ambaye anashiriki kama mshiriki mwandamizi katika Gasshuku (semina kuu) ya Jundokan Karate ya nchi za Ulaya inayofanyika São Domingos de Rana, Lisbon, nchini Portugal kuanzia Juni 19 hadi 21, 2026.
Ushiriki wa Sensei Rumadha unaendelea kuiwakilisha vyema Tanzania katika mkusanyiko huo mkubwa unaowakutanisha wakufunzi na wachezaji wa karate kutoka mataifa mbalimbali ya Ulaya na kwingineko duniani.
Semina hiyo inaongozwa na mabingwa wa kiwango cha juu wa Jundokan Karate, akiwemo Tetsu Gima mwenye Dan ya 10 na Tsuneo Kinjo, wote kutoka makao makuu ya Jundokan So Hombu yaliyopo Okinawa nchini Japan.
Mafunzo hayo pia yanasaidiwa na Takayuki Miyakozawa na Hirokazu Aono, huku mgeni maalum akiwa Degracias Medina, mwenye Dan ya 9 katika Shito-Ryu Karate.
Ushiriki wa Sensei Rumadha katika semina hiyo unadhihirisha hatua kubwa ya maendeleo ya karate nchini Tanzania na kuimarisha uhusiano wa kimafunzo kati ya Tanzania na jumuiya ya karate ya kimataifa. Kupitia jukwaa hilo, Tanzania inaendelea kujenga heshima na kutambulika zaidi katika mchezo wa karate duniani.