
Mtanzania Rahma Warioba amefunguka kuhusu changamoto na mateso aliyodai kuyapitia nchini Oman, ambako bado anafanya kazi za ndani.
Rahma ameeleza safari yake tangu alipoondoka Tanzania hadi kufika Oman, akisimulia mazingira magumu ya kazi aliyokutana nayo kwa waajiri wake. Miongoni mwa changamoto alizozitaja ni kufanya kazi nyingi za nyumbani huku akihudumia familia yenye takribani watu 10, ambapo alidai kupata saa moja tu ya kupumzika kwa siku.
Aidha, amesema mshahara wake uliwahi kukatwa baada ya kuunguza nguo ya mwajiri wake alipokuwa akipiga pasi. Pia ameeleza jinsi alivyoamua kuondoka kwa mwajiri wake na baadaye kusaidiwa na mtu aliyemtaja kwa jina la Masoud.
Kufuatia simulizi ya Rahma kuhusu changamoto hizo, Masoud, ambaye pia anajihusisha na kuwatafutia kazi wasichana wanaokwenda kufanya kazi nchini Oman, amefunguka na kueleza upande wake wa tukio hilo.
Masoud amezungumzia mazingira halisi ya kazi za ndani nchini Oman, changamoto zinazowakabili baadhi ya wafanyakazi wa ndani, pamoja na namna alivyohusika katika kumsaidia Rahma baada ya kuondoka kwa mwajiri wake.
Vilevile, ametoa ushauri kwa Watanzania wanaotarajia kwenda kufanya kazi nje ya nchi, akisisitiza umuhimu wa kupata taarifa sahihi kuhusu mazingira ya kazi, haki zao na changamoto zinazoweza kujitokeza ili waweze kufanya maamuzi sahihi kabla ya kuanza safari zao.