Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na mfululizo wa matetemeko makubwa ya ardhi yaliyolikumba pwani ya kaskazini mwa Venezuela imeongezeka hadi 164, huku 971 wakijeruhiwa, kwa mujibu wa Kaimu Rais wa nchi hiyo, Delcy Rodríguez.
Tetemeko hilo lenye ukubwa wa 7.5 katika kipimo cha Richter lilitokea sekunde 39 baada ya tetemeko la awali lenye ukubwa wa 7.2, na kuwa tetemeko lenye nguvu zaidi kuikumba Venezuela katika kipindi cha zaidi ya miaka 100.
Wakati shughuli za uokoaji zikiendelea na picha kutoka maeneo yaliyoathirika zikiendelea kuibuka, mamlaka zimeonya kuwa idadi ya vifo na majeruhi huenda ikaongezeka zaidi.
Wakazi wa mji mkuu, Caracas, wameelezea ukubwa wa maafa hayo kuwa haujawahi kushuhudiwa. Mkazi mmoja aliyenusurika alisema hata tetemeko kubwa la mwaka 1967 halikufanana na janga hili, huku mwingine aliyefanikiwa kutoka kwenye jengo lililoharibiwa akisema, “Mandhari ilikuwa kama filamu ya kutisha.”
Nchini Marekani, Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio amesema tayari timu za uokoaji zimepelekwa Venezuela, huku vifaa na rasilimali zaidi vikitarajiwa kuwasili kupitia uwanja mkuu wa ndege wa nchi hiyo, ambao amesema umeharibika vibaya.
Janga hilo limeikumba Venezuela katika kipindi ambacho tayari inakabiliwa na changamoto kubwa za kisiasa na kiuchumi. Delcy Rodríguez amesema serikali inashirikiana na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuanzisha mfuko wa awali wa msaada wenye thamani ya dola milioni 200 kwa ajili ya kukabiliana na athari za maafa hayo.