Kipa mkongwe wa Cape Verde, Vozinha, ameendelea kuandika historia katika Kombe la Dunia 2026 baada ya kuiongoza timu yake kutinga hatua ya mtoano huku ikiwa haijapoteza mchezo wowote katika hatua ya makundi.
Katika mchezo wa kwanza dhidi ya Hispania, Vozinha mwenye umri wa miaka 40 aliwashangaza wengi duniani baada ya kuichezea Cape Verde kwa mara ya kwanza katika Kombe la Dunia na kufanikiwa kumaliza mchezo bila kuruhusu bao.
Hata hivyo, furaha yake haikuwa kamili, kwani mama yake hakuweza kushuhudia tukio hilo kutokana na changamoto za kupata visa.
Baada ya mechi hiyo ya kihistoria, changamoto hizo zilitatuliwa na mama yake akapata nafasi ya kusafiri na kumshuhudia mwanawe akiandika historia tena, baada ya kutoruhusu bao kwa mara nyingine na kuisaidia Cape Verde kutinga hatua ya 16 bora.
Katika kila shuti alilookoa Vozinha, mama yake alionekana akishangilia kwa hisia kubwa kana kwamba timu yake imefunga bao, jambo lililogusa mioyo ya mashabiki wengi wa soka duniani.
Baada ya mchezo, mama na mwana walikutana na kusherehekea mafanikio hayo pamoja, tukio lililokuwa la kihisia kwa familia yao na taifa zima la Cape Verde.
Ikiwa na idadi ya watu takribani 530,000, Cape Verde imeweka rekodi ya kuwa taifa lenye idadi ndogo zaidi ya watu kuwahi kufuzu hatua ya mtoano katika historia ya Kombe la Dunia.
Licha ya kupangwa kundi moja na Hispania, Uruguay na Saudi Arabia, wengi hawakuwapa nafasi ya kufanya vizuri. Hata hivyo, Cape Verde imewashangaza wengi kwa kumaliza hatua ya makundi bila kupoteza mchezo hata mmoja.
Sasa Cape Verde inajiandaa kuvaana na mabingwa watetezi, Argentina, katika hatua ya 16 bora, huku ikiendelea kuandika moja ya simulizi za kuvutia zaidi za Kombe la Dunia 2026.