
Timu ya taifa ya Morocco imefuzu hatua ya 16 Bora ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kuiondoa Uholanzi kwa ushindi wa penalti 3-2, kufuatia sare ya 1-1 iliyodumu hadi mwisho wa dakika 120 katika mchezo mkali uliochezwa mjini Monterrey.
Mchezo huo ulianza kwa kasi kubwa huku timu zote zikitengeneza nafasi kadhaa za kufunga. Morocco ilionekana kuwa na nafasi nzuri zaidi kipindi cha kwanza, lakini ilishindwa kuzitumia kupitia Ismael Saibari, Achraf Hakimi na Azzedine Ounahi, huku kipa wa Uholanzi Bart Verbruggen akiokoa hatari kadhaa.
Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika bila mabao, Morocco iliendelea kushambulia kipindi cha pili lakini ilijikuta ikiruhusu bao dakika ya 72 kupitia Cody Gakpo, aliyemalizia pasi ya Crysencio Summerville kufuatia shambulizi la kushtukiza.
Morocco ilionyesha moyo wa kupambana hadi dakika za mwisho, ambapo Issa Diop aliisawazishia timu hiyo bao la kichwa katika muda wa nyongeza wa kipindi cha pili baada ya kupokea krosi ya Chemsdine Talbi na kupeleka mchezo huo katika dakika 30 za nyongeza.
Katika muda wa nyongeza, timu zote zilipata nafasi za kufunga lakini walinzi na makipa walifanya kazi kubwa kuhakikisha hakuna timu inayopata bao la ushindi, hivyo mshindi akapatikana kwa mikwaju ya penalti.
Katika hatua ya penalti, Neil El-Aynaoui alianza kwa kukosa kwa Morocco huku Justin Kluivert pia akikosa kwa Uholanzi. Soufiane Rahimi alifunga penalti yake licha ya kipa Verbruggen kuigusa, kabla ya Quentin Timber kupiga nje penalti ya nne ya Uholanzi.
Achraf Hakimi alipata nafasi ya kuiweka Morocco mbele lakini akagonga mwamba, kabla ya kipa Yassine Bounou kuibuka shujaa kwa kuokoa penalti ya Crysencio Summerville. Ismael Saibari ndiye aliyefunga penalti ya mwisho kwa utulivu na kuipa Morocco ushindi wa 3-2.
Kwa ushindi huo, Morocco imefuzu hatua ya 16 Bora na sasa itakutana na Canada Julai 4 mjini Houston, ikiendelea kufufua matumaini ya kufanya safari nyingine ya kihistoria katika Kombe la Dunia 2026.