
Rhoda Chacha Mwita, Mtanzania aliyesafiri kwenda India mwaka 2017 baada ya kuahidiwa kazi ya hoteli iliyodaiwa kubadili maisha yake, amesema alijikuta akiingizwa kwenye shughuli haramu tofauti na alivyokuwa ameahidiwa.
Rhoda amesema mara tu alipowasili nchini India, bosi wake alimnyang’anya hati yake ya kusafiria (passport) na kumlazimisha kufanya kazi hiyo haramu kwa madai ya kulipa deni alilokuwa akidaiwa.
Amesema baada ya kuvumilia kwa muda, aliamua kumpinga mwajiri wake jambo lililosababisha kutishiwa kuuawa. Kutokana na hofu hiyo, aliamua kuripoti tukio hilo kwa polisi, ambao walimkamata bosi huyo.
Akizungumzia maisha yake nchini India, Rhoda amesema alipata mtoto mmoja akiwa huko na raia wa Tanzania, lakini baba wa mtoto huyo alifukuzwa nchini India na kurejeshwa Tanzania.
Rhoda amesema anajutia uamuzi wa kusafiri kwenda India kwa ahadi za kazi ambazo baadaye zilibainika kuwa si za kweli.
Amewataka mabinti wa Kitanzania wanaopanga kwenda kutafuta kazi nje ya nchi kuhakikisha wanathibitisha uhalali wa ajira wanazoahidiwa na kuchukua tahadhari zote muhimu, akisisitiza kuwa ahadi nyingi za kazi zinazotolewa kupitia mawakala wasio waaminifu huishia kuwa chanzo cha mateso na madhara makubwa.