×

TIPER Yaweka Rekodi Mpya, Yampa Rais Samia Gawio la Bilioni 15

Rais wa Jamhuri ya Muungwana wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan (katikati)akikabidhi Tuzo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tiper Balozi Mathias Chikawe(kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Tiper Mohamed Mohamed (kulia) wakati wa hafla ya Siku ya Gawio ambapo TIPER imekabidhi gawio la Sh.Bilioni 15 kwa Rais Samia jana Juni 30,Ikulu jijini Dar es Salaam

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amepokea gawio la Shilingi bilioni 15 kutoka Kampuni ya Kuhifadhi Mafuta Tanzania (TIPER), ikiwa ni sehemu ya gawio la jumla la Shilingi bilioni 30 lililotolewa kwa wanahisa wawili wa kampuni hiyo.

Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina inamiliki asilimia 50 ya hisa za TIPER, huku Oryx Energies Tanzania ikimiliki asilimia 50 iliyobaki.

Akizungumza katika hafla ya Siku ya Gawio Ikulu, Dar es Salaam, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, amesema hilo ndilo gawio kubwa zaidi kuwahi kutolewa na TIPER, akieleza mafanikio hayo yanaonyesha kuimarika kwa utendaji wa kampuni.

Mkurugenzi Mtendaji wa TIPER, Mohamed Mohamed, amesema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji katika miundombinu, ufanisi wa uendeshaji na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyojengwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia.

Rais wa Jamhuri ya Muungwana wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan (katikati) akikabidhiwa gawio la Sh.bilioni 15 kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tiper Balozi Mathias Chikawe (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Tiper Mohamed Mohamed (kulia) wakati wa hafla ya Siku ya Gawio iliyofanyika Ikulu Dar es Salaam ambapo mashirika na taasisi mbalimbali ambazo Serikali inahisa wamekabidhi gawio serikalini.

Amesema kati ya mwaka 2016 na 2020 Serikali ilipokea gawio la Shilingi bilioni 7.65, lakini kati ya mwaka 2021 na 2025 gawio liliongezeka hadi Shilingi bilioni 30.65.

Aidha, gawio la Serikali limeongezeka kutoka Shilingi milioni 500 mwaka 2021 hadi Shilingi bilioni 15 mwaka 2025.

Mohamed amesema mapato hayo yanasaidia kugharamia utekelezaji wa bajeti ya Serikali na huduma za maendeleo ikiwemo barabara, hospitali, shule na miradi ya umeme.

Ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita TIPER imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 105 kuboresha matanki ya kuhifadhi mafuta, mifumo ya usambazaji, kuzima moto na umeme, hatua iliyoongeza uwezo wa kuhifadhi mafuta kutoka lita milioni 253 hadi milioni 313.

Pia amesema kuanza kwa mfumo wa Single Receiving Terminal (SRT) wa mafuta ya dizeli Januari 2025 kumepunguza muda wa meli kupakua mafuta kutoka wastani wa siku tisa hadi siku nne na kuongeza ufanisi wa shughuli za bandari.

Ameongeza kuwa TIPER imepanga kuwekeza zaidi ya Shilingi bilioni 265 katika kipindi cha miaka mitano ijayo ili kuongeza uwezo wa kuhifadhi na kusafirisha mafuta, kuimarisha usalama wa nishati na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya mafuta Afrika Mashariki na Kati.

Leave a Comment