×

Equity Group Yawaunganisha Wawekezaji wa Kimataifa na Sekta Binafsi Tanzania

Equity Group imeongoza ziara ya siku nne ya Biashara na Uwekezaji nchini Tanzania Bara na Zanzibar, ikiwaleta pamoja wawekezaji, wafanyabiashara na viongozi wa biashara kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika na nje ya bara hilo ili kutafuta fursa mpya za uwekezaji na ushirikiano wa kibiashara.

Ziara hiyo, iliyofanyika kuanzia Juni 29 hadi Julai 2, 2026, imelenga kuonesha uwezo wa Tanzania kama moja ya chumi zinazokua kwa kasi zaidi Afrika Mashariki na kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya sekta binafsi za nchi mbalimbali.

Katika hatua muhimu ya ziara hiyo, Equity Group kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), iliandaa Kongamano la Biashara lililofanyika katika Ukumbi wa Mfalme kwenye viwanja vya Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo liliwakutanisha wawekezaji wa kimataifa, wafanyabiashara wa ndani na viongozi wa Serikali kwa lengo la kujadili fursa za biashara, uwekezaji na maendeleo ya viwanda, huku likitoa nafasi ya kujenga ushirikiano mpya wa kibiashara.

Akizungumza wakati wa kongamano hilo, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Sempeho Manongi, alisema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuvutia mitaji zaidi na kuharakisha ukuaji wa sekta binafsi pamoja na viwanda.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wateja Wadogo, wa Kati na Binafsi wa Equity Bank Tanzania, Bi. Theresia Mayanie, alisema benki hiyo inaendelea kuwa kiungo muhimu kati ya wawekezaji na fursa zilizopo nchini kupitia huduma za ushauri wa biashara, fedha za biashara, ubadilishaji wa fedha za kigeni na mwongozo wa kisheria.

Naye Mkurugenzi wa Mahusiano ya Biashara wa Equity Group, Bw. AQ Hamza, alisema misafara ya biashara imeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kukuza uchumi kwa kuunganisha wafanyabiashara, kujenga ushirikiano wa muda mrefu na kuwezesha biashara za kuvuka mipaka.

Aidha, Mkurugenzi wa Ukuzaji wa Biashara wa TanTrade, Bw. Jonathan Nkwabi, aliwasilisha fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji zinazopatikana Tanzania, kabla ya washiriki wa ziara hiyo kutembelea Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba na kujionea bidhaa, huduma na sekta mbalimbali za uzalishaji zinazochochea ukuaji wa uchumi wa nchi.

Ziara hiyo inatarajiwa kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na masoko ya kimataifa, huku ikifungua fursa mpya za uwekezaji, biashara na ushirikiano kwa sekta binafsi.

Leave a Comment