×

Waziri Mkuu Atoa Wito wa Kutafuta Njia Mpya za Kueneza Kiswahili Duniani

Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema kuna umuhimu wa kubuni mbinu mpya za kukieneza Kiswahili duniani baada ya lugha hiyo kuendelea kupata umaarufu na hadhi ya kimataifa.

Akizungumza Jumanne, Julai 7, 2026, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Tano ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika katika makao makuu ya UNESCO jijini Paris, Ufaransa, Waziri Mkuu alisema hatua inayofuata ni kuhakikisha Kiswahili kinaendelea kusambaa zaidi kupitia mikakati ya kisasa.

Alisema mataifa mengi yamefanikiwa kueneza lugha na utamaduni wao duniani kupitia vituo vya utamaduni vilivyoanzishwa katika nchi mbalimbali, hivyo kuna haja ya kuangalia uwezekano wa kutumia njia kama hizo kwa Kiswahili.

“Kadiri Kiswahili kinavyoendelea kupata hadhi ya kimataifa, ni muhimu sasa kuanza kutazama hatua inayofuata ya kukieneza duniani,” alisema Dkt. Nchemba.

Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea kuimarisha matumizi ya Kiswahili ndani na nje ya nchi kupitia elimu, tafiti, uchapishaji, tafsiri, teknolojia za kidijitali na diplomasia ya lugha.

Aliongeza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na UNESCO, nchi mbalimbali, vyuo vikuu na taasisi za kimataifa katika kuhakikisha Kiswahili kinaendelezwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Dkt. Nchemba, aliyekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema Kiswahili tayari kimepata nafasi muhimu kimataifa baada ya kutambuliwa kuwa lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na kuwa miongoni mwa lugha rasmi za Umoja wa Afrika (AU).

“Kiswahili ndiyo utambulisho wetu wana jumuiya ya Afrika Mashariki. Mtu akiongea Kiswahili anajulikana kuwa anatokea Tanzania, Burundi, Congo au Sudan Kusini,” alisema.

Kwa mujibu wa wataalamu wa lugha, Kiswahili kinazungumzwa na watu kati ya milioni 300 hadi 500 duniani, huku matumizi yake yakiendelea kuongezeka kupitia elimu, biashara, vyombo vya habari, teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na mitandao ya kijamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Prof. Khaled El-Enany, alisema shirika hilo limeunga mkono uandaaji wa kamusi ya Kifaransa kwenda Kiswahili, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa kwa walimu, wanafunzi na watu wanaojifunza lugha hizo mbili.

Leave a Comment