×

Kiungo wa Uingereza Afanyiwa Upasuaji Baada ya Kuumia Kombe la Dunia

Kiungo wa timu ya taifa ya Uingereza, Jordan Henderson, amewapa mashabiki taarifa mpya kuhusu hali yake ya kiafya baada ya kufanyiwa upasuaji kutokana na jeraha kubwa la mkono lililomfanya kuikosa michuano ya Kombe la dunia 2026.

Henderson alisafirishwa kurejea Kansas City, ambako kikosi cha Uingereza kimeweka kambi, kabla ya kufanyiwa upasuaji baada ya kutangazwa kuwa hatoweza kuendelea kucheza katika mashindano hayo.

Baada ya upasuaji huo, nyota huyo mwenye umri wa miaka 36 alichapisha picha akiwa hospitalini akiwa na bandeji mkononi na kutoa ujumbe wa kuwapa matumaini mashabiki.

“Upasuaji umekamilika! Tuwe tayari kwa mchezo mkubwa wa Jumamosi. Asante kwa wafanyakazi wote walionihudumia katika Kansas City Orthopaedic Institute, hasa madaktari watatu waliofanya upasuaji,” aliandika Henderson.

Henderson aliwashukuru madaktari Kenneth P. Unruh, Mark J. Winston na Kirk McCullough kwa msaada waliompa.

Ingawa hatoweza kucheza tena katika Kombe la Dunia, Henderson ataendelea kubaki na kikosi cha England hadi mwisho wa mashindano, akiwa sehemu muhimu ya usaidizi kwa wachezaji wenzake.

Jeraha hilo lilitokea baada ya ushindi wa Uingereza dhidi ya Mexico, ambapo Henderson alianguka baada ya kuruka uzio wa matangazo wakati wa kusherehekea ushindi huo mkubwa. Alihitaji kubebwa kwa machela na kupewa huduma ya haraka kabla ya kupelekwa hospitalini.

Licha ya kutocheza tena, Henderson anaendelea kuwa mmoja wa wachezaji wenye ushawishi mkubwa ndani ya kikosi cha kocha Thomas Tuchel. Wachezaji wengi akiwemo Jude Bellingham wamempa moyo baada ya tukio hilo.

Beki wa England Marc Guéhi alisema hali ya Henderson imeimarika na kwamba tukio hilo lilikuwa la kuogopesha kwa mchezaji huyo, familia yake na kikosi kizima.

Uingereza inajiandaa kwa mchezo wa robo fainali dhidi ya Norway Jumamosi, huku Henderson akiwa pembeni akitoa sapoti kwa wenzake katika harakati za kutafuta taji la dunia.

Leave a Comment