
TEHRAN – Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vimeripoti kuwa Marekani imefanya mashambulizi yaliyolenga maeneo ya pembezoni mwa kinu pekee cha nyuklia cha matumizi ya kiraia nchini humo kilichopo Bushehr.
Naibu Gavana wa Mkoa wa Bushehr, Ehsan Jahanian, alisema maeneo kadhaa yalilengwa, yakiwemo eneo la kuzunguka kinu hicho cha nyuklia, kambi ya kijeshi katika mji wa Choghadak na gati la wavuvi kusini mwa mkoa huo. Alisema hadi wakati huo hakukuwa na taarifa za vifo au majeruhi.
Wakazi wa Choghadak, uliopo takribani kilomita 20 kutoka kinu cha Bushehr, waliripoti kusikia milipuko kadhaa. Hii si mara ya kwanza mashambulizi kuripotiwa karibu na eneo hilo.
Mwezi Aprili, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) lilionya kuwa mashambulizi yanayofanyika karibu na kinu hicho yanaweka usalama wa nyuklia katika hatari kubwa na yanapaswa kusitishwa mara moja.
Kituo cha Bushehr kilijengwa kwa ushirikiano wa Urusi na kwa sasa kina mtambo mmoja unaofanya kazi huku mingine miwili ikiwa katika hatua za ujenzi. Wakati wa vita vya awali, Urusi iliwahamisha wataalamu wake kutoka eneo hilo kwa sababu za kiusalama.
Ripoti hiyo imeibuka wakati mapigano mapya kati ya Marekani na Iran yakizidi kuongezeka, huku yakihusishwa na mvutano kuhusu Mlango wa Hormuz, hali ambayo imeibua hofu ya kurejea kwa vita kamili licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa miezi iliyopita.
Maafisa wa Iran walisema mashambulizi ya Marekani yaliyodumu kwa siku mbili yamesababisha vifo vya watu 17. Serikali ya Iran pia ilitangaza kuendelea na mashambulizi dhidi ya mali na vituo vya Marekani katika nchi za Kuwait, Bahrain na Qatar.
Jeshi la Jordan lilisema lilifanikiwa kudungua makombora manane yaliyorushwa kutoka Iran kuelekea maeneo ya washirika wa Marekani katika ukanda huo.
Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilishutumu mashambulizi ya Marekani kwa kulenga miundombinu ya kiraia, ikiwemo madaraja ya reli, na kuyataja kama “uhalifu mkubwa wa kivita.”
Kwa upande wake, maafisa wa jeshi la Marekani walidai kuwa mashambulizi ya Alhamisi yalilenga takribani maeneo 90 ya kijeshi nchini Iran, yakiwemo mifumo ya ulinzi wa anga, maghala ya makombora na vituo vya kuhifadhi ndege zisizo na rubani (drones).
Jeshi la Iran nalo lilisema lilishambulia mfumo wa makombora ya Patriot nchini Kuwait, mfumo wa tahadhari ya mapema nchini Qatar pamoja na matangi ya mafuta nchini Bahrain kwa kutumia ndege zisizo na rubani, kama sehemu ya operesheni zake dhidi ya vituo vya Marekani katika eneo la Ghuba.