×

Kisa cha Kusikitisha: Mwanamke Afanya Mauaji Kisa Wivu wa Mapenzi, Afungwa Maisha

Aliyehukumiwa kifungo cha maisha, Sakiyna Thompson (kushoto) mwenye umri wa miaka 31 na Kulia ni Kayla Hodgson mwenye umri wa miaka 23 enzi za uhai wake.

Tamarac, Florida, Marekani — Mahakama nchini Marekani ilimhukumu, Sakiyna Thompson mwenye umri wa miaka 31 kifungo cha maisha jela bila uwezekano wa kuachiwa huru baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mwanamke aliyekuwa akihusishwa kimapenzi na aliyekuwa mpenzi wake wa zamani.

Thompson alihukumiwa Jumatatu, Desemba 1, 2025 baada ya mwezi Oktoba kupatikana na hatia ya mauaji ya daraja la kwanza ya Kayla Hodgson mwenye umri wa miaka 23, tukio lililotokea Julai mwaka 2022 katika eneo la Tamarac, Florida.

Kwa mujibu wa waendesha mashtaka, Thompson alisafiri kutoka New York hadi South Florida siku chache kabla ya tukio hilo akiwa na mpango wa kumuua Kayla, ambaye walidai alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mwanaume aliyewahi kuwa mpenzi wa Sakiyna.

Mashtaka yalieleza kuwa Sakiyna alifika kwenye nyumba ya Kayla, mapema asubuhi majira ya saa 5, kisha alimkabili kuhusu uhusiano wao na mwanaume huyo kabla ya tukio hilo kusababisha kifo cha Kayla.


Mashtaka Yadai Mauaji Yalipangwa

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuwa Sakiyna hakufanya tukio hilo kwa bahati mbaya, bali alikuwa amelifanyia maandalizi.

Walidai kuwa Thompson alijaribu kuficha utambulisho wake kwa kuvaa kofia na barakoa wakati wa kwenda kwenye eneo la tukio, na pia alitumia akaunti bandia ya Uber kwa safari yake ya kwenda na kurudi hotelini.

Baada ya uchunguzi na ushahidi uliowasilishwa mahakamani, majaji walifikia uamuzi wa kumtia hatiani baada ya majadiliano ya takribani saa moja pekee.

Utetezi Wadai Alikuwa Akijilinda

Kwa upande mwingine, mawakili wa Sakiyna walidai kuwa tukio hilo halikuwa mauaji yaliyopangwa, bali lilitokea wakati wa mapambano ambapo Sakiyna alikuwa akijilinda.

Walieleza kuwa Hodgson ndiye aliyeanzisha shambulio hilo na kwamba Sakiyna alipata majeraha wakati wa mapambano hayo. Pia walidai Sakiyna alipoteza fahamu wakati wa tukio na hakukumbuka kikamilifu kilichotokea.

Hata hivyo, waendesha mashtaka walipinga maelezo hayo na kusema ushahidi uliopo ulionyesha kuwa Thompson alikuwa na nia ya kumuua Hodgson.

Familia ya Kayla Mahakamani

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, ndugu na marafiki wa Kayla walizungumza mahakamani wakieleza maumivu waliyopitia tangu kupoteza mpendwa wao.

Melanie John, mmoja wa ndugu wa Kayla, alisema kitendo hicho kilikuwa cha kikatili na kwamba mtu aliyefanya uhalifu huo hakupaswa kupewa nafasi nyingine ya kutoka na kuendelea na maisha yake.

Ndugu mwingine, Alisha Mitchell, alisema hukumu hiyo imewasaidia kuanza mchakato wa kupona, ingawa pengo la kumpoteza Kaylalitaendelea kuwepo.

Hukumu ya Mwisho

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, mahakama iliamua kutoa adhabu ya kifungo cha maisha bila uwezekano wa msamaha kwa Sakiyna.

Uamuzi huo umehitimisha kesi iliyodumu kwa zaidi ya miaka miwili tangu tukio la mwaka 2022, huku familia ya Hodgson ikisema sasa wanapata angalau hisia ya haki baada ya aliyesababisha kifo cha mpendwa wao kuwajibishwa.

Leave a Comment