×

Simanzi Chalinze! Watoto Watatu Wakutwa Wamefariki Ndani ya Gari

Huzuni imetanda katika Kijiji cha Lamboni, Kata ya Lugoba, Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani, baada ya watoto watatu waliokuwa wameripotiwa kupotea kukutwa wamefariki dunia ndani ya gari bovu lililokuwa limeegeshwa katika eneo la makazi.

Watoto hao wametambulika kuwa ni Masoud Mwema (9), Mikidadi Halfani (4) na Murath Mbaraka (4).

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, miili ya watoto hao iligunduliwa Julai 10, 2026 majira ya saa 1:30 usiku na kijana aitwaye Lilahi Mgaza (19), ambaye alikuwa akikagua magari yaliyokuwa yameegeshwa nje ya nyumba wanayoishi.

Kamanda Morcase amesema watoto hao walikutwa ndani ya gari aina ya Toyota Carina TI lenye namba za usajili T 116 CJV, huku milango na madirisha ya gari hilo yakiwa yamefungwa.

Ameeleza kuwa wazazi wa watoto hao walitoa taarifa ya kupotea kwa watoto wao katika Kituo cha Polisi Julai 9, 2026 baada ya kushindwa kuwaona tangu walipotoweka.

Miili ya watoto hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Msoga kwa ajili ya uchunguzi zaidi, huku Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi wa kubaini mazingira halisi yaliyosababisha vifo hivyo.

Kamanda Morcase amewataka wananchi kuwa watulivu wakati uchunguzi ukiendelea, na ametoa wito kwa wazazi na walezi kuendelea kufuatilia kwa karibu maeneo wanayochezea watoto ili kuzuia matukio ya aina hiyo kujirudia.

Leave a Comment