×

Trump Aitishia Iran Ikijaribu Kumuua Atajibu kwa Nguvu Kubwa

Rais wa Marekani, Donald Trump, ameionya serikali ya Iran kwamba Marekani itachukua hatua kali za kijeshi endapo kutakuwa na jaribio lolote la kuhatarisha maisha yake au kumuua.

Kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, Trump alisema Marekani ina uwezo mkubwa wa kijeshi tayari na kwamba hatua kali zitachukuliwa ikiwa Iran itatekeleza tishio lolote dhidi yake.

“Makombora elfu moja yako tayari na yameelekezwa kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ikiwa tishio la serikali ya Iran la kumuua Rais wa Marekani litatekelezwa, makombora zaidi ya elfu moja yatafyatuliwa mara moja,” Trump aliandika.

Trump pia alisema ametoa maagizo yanayohitajika na kwamba jeshi la Marekani liko tayari kuchukua hatua za kulenga maeneo mbalimbali nchini Iran endapo hali hiyo itatokea.

Kauli hiyo imekuja baada ya ripoti za kijasusi kutoka Israel kudai kuwa huenda kulikuwa na mpango mpya wa Iran wa kutaka kumuua Trump, pamoja na kauli na picha zilizoonekana wakati wa mazishi ya aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei.

Hata hivyo, viongozi wa Iran wamekanusha madai hayo na kusema hakuna mpango wowote wa kumuua rais huyo wa Marekani.

Mvutano kati ya Marekani na Iran umeendelea kuongezeka katika kipindi cha hivi karibuni kutokana na mashambulizi ya kijeshi, masuala ya usalama na mvutano wa kisiasa kati ya mataifa hayo mawili.

Leave a Comment