
Nahodha wa Argentina, Lionel Messi, anatarajiwa kuandika historia mpya Jumatano atakapoiongoza timu yake kuivaa England katika nusu fainali ya Kombe la Dunia 2026, ikiwa ni mara yake ya kwanza kabisa kucheza dhidi ya taifa hilo katika maisha yake ya soka ya kimataifa.

Kwa zaidi ya miaka 20, Messi amewahi kucheza dhidi ya mataifa mengi yaliyowahi kutwaa Kombe la Dunia, yakiwemo Brazil, Ujerumani, Italia, Hispania na Ufaransa, lakini hajawahi kukutana na England katika mechi ya kimataifa.
Shirikisho la Soka la Argentina (AFA) limeitaja mechi hiyo kuwa ni “mchezo ambao hatima ilikuwa imemuandikia Messi,” kutokana na kusubiriwa kwake kwa muda mrefu.
Messi mwenye umri wa miaka 39 alisema baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Uswisi katika robo fainali kuwa England ni moja ya timu kubwa duniani na ni heshima kucheza mechi ya kiwango hicho.
“Ni mechi maalum kwa sababu England ni timu kubwa. Tunahitaji kupumzika na kujiandaa vizuri ili tuendelee kupambana kama tulivyofanya hadi sasa,” alisema Messi.
Argentina imefika nusu fainali baada ya kupitia safari ngumu katika hatua za mtoano, ikiwafunga Cape Verde na Misri kwa mabao 3-2 kabla ya kuiondoa Uswisi kwa mabao 3-1 baada ya muda wa nyongeza.
Dhidi ya Uswisi, Messi alitoa pasi ya bao la kwanza lililofungwa na Alexis Mac Allister, ingawa hiyo ilikuwa mechi yake ya kwanza ya Kombe la Dunia tangu mwaka 2022 kutofunga bao.
Mchuano kati ya Argentina na England unatarajiwa kuwa moja ya mechi zenye ushindani mkubwa kutokana na historia ndefu ya uhasama wa kisoka kati ya mataifa hayo mawili, huku mshindi akitinga fainali ya Kombe la Dunia 2026.