
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma (PSRS), kwa niaba ya Tume ya Ushindani wa Haki (Fair Competition Commission – FCC) na Chuo cha Taifa cha Utalii (National College of Tourism – NCT), imetangaza nafasi 22 za ajira kwa Watanzania wenye sifa, uwezo na weledi wa kufanya kazi katika taasisi hizo.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, FCC inahitaji kujaza nafasi za Maafisa Ufuatiliaji wa Bidhaa Bandia Daraja la II (Counterfeit Surveillance Officer II) pamoja na Maafisa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Daraja la II (ICT Officer II – Computer System Security), ambapo kila kada ina nafasi mbili.
Kwa upande wa Maafisa Ufuatiliaji wa Bidhaa Bandia, waombaji wanatakiwa kuwa na Shahada ya Utekelezaji wa Sheria (Law Enforcement) kutoka chuo kinachotambuliwa. Majukumu yao yatakuwa ni pamoja na kufuatilia bidhaa bandia katika mipaka, maduka na maghala, kufanya ukaguzi na misako, kukamata bidhaa zinazoshukiwa kuwa bandia, kuchukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi wa maabara pamoja na kuandaa taarifa za uchambuzi wa shughuli hizo.
Kwa nafasi za Maafisa wa ICT, waombaji wanapaswa kuwa na Shahada katika fani zinazohusiana na Sayansi ya Kompyuta, Uhandisi wa Kompyuta, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), Usalama wa Mifumo ya Kompyuta, Uhandisi wa Mitandao au taaluma nyingine zinazolingana. Watahusika kusimamia mifumo ya TEHAMA, kuimarisha usalama wa mifumo ya kompyuta, kutekeleza sera za TEHAMA pamoja na kushiriki katika matengenezo na maboresho ya mifumo ya kiteknolojia ya taasisi.
Aidha, Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) kimetangaza nafasi za Katibu Muhtasi Daraja la II (Office Management Secretary Grade II). Waombaji wa nafasi hizo wanapaswa kuwa na Stashahada ya Uhazili (Ordinary Diploma – NTA Level 6) kutoka chuo kinachotambuliwa. Majukumu yao ni pamoja na kuandaa na kuchapa nyaraka mbalimbali, kuratibu mikutano, kuhifadhi kumbukumbu za nyaraka na mafaili, kupokea wageni na simu, pamoja na kutekeleza majukumu mengine ya kiutawala watakayopangiwa.
Sekretarieti ya Ajira imewataka waombaji wote kuhakikisha wanakidhi vigezo vilivyowekwa katika tangazo rasmi na kuwasilisha maombi yao kupitia mfumo wa kielektroniki wa Ajira kwa kuzingatia masharti yaliyotolewa.
Soma zaidi bonyeza hapa chini
NAFASI ZA KAZI CHUO CHA TAIFA CHA UTALII NA TUME YA USHINDANI 14-07-2026