×

Lamine Yamal Atoa Ujumbe Mzito Kabla ya Kukiwasha na Ufaransa leo

Nyota wa timu ya taifa ya Hispania, Lamine Yamal, amesema soka inapaswa kuwa daraja la kuwaleta watu pamoja badala ya kutumiwa kuleta tofauti, wakati timu yake ikijiandaa kukutana na Ufaransa katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia 2026 leo saa nne usiku.

Kauli hiyo ya Yamal imekuja baada ya kuulizwa kuhusu kauli iliyowahi kutolewa na Waziri Mkuu wa zamani wa Hispania, Mariano Rajoy, kuhusu timu ya Ufaransa, akidai kuwa ni timu kubwa lakini “haina wachezaji wengi wa Kifaransa.”

Yamal, ambaye ni mtoto wa baba mwenye asili ya Morocco na mama mwenye asili ya Guinea ya Ikweta, alisema historia yake ni mfano wa jinsi soka linavyoweza kuonyesha nguvu ya mchanganyiko wa tamaduni mbalimbali.

“Kesho tutacheza mchezo mkubwa, lakini kama kuna jambo ambalo soka linaweza kufanya ni kuwaunganisha watu. Hispania na Ufaransa ni mifano ya mshikamano na ujumuishaji. Hilo ndilo soka linahusu,” alisema Yamal.

Kauli hiyo ilitolewa wakati Yamal akitimiza miaka 19, huku akiwa katika kipindi ambacho umaarufu wake umeongezeka kutokana na uwezo wake uwanjani na matarajio makubwa aliyonayo katika michuano hiyo.

Katika mkutano na waandishi wa habari, Yamal pia alizungumzia mdogo wake Keyne mwenye umri wa miaka mitatu, ambaye amekuwa kivutio kwa mashabiki baada ya kuonekana mara kadhaa mbele ya kamera wakati wa mashindano.

Yamal alisema mdogo wake huwa anafanya mambo ya kawaida akiwa nyumbani, lakini anapokutana na kamera huonyesha tabia yake ya kuchekesha na kuwafurahisha watu.

Mbali na hayo, mshambuliaji huyo alionekana akiwa amevaa mkufu mkubwa wa almasi ambao ulikuwa zawadi yake ya siku yake ya kuzaliwa, huku akisema mchezo dhidi ya Ufaransa ndio muhimu zaidi katika maisha yake ya soka hadi sasa.

Licha ya kufunga bao moja pekee katika Kombe la Dunia 2026, Yamal amesema hana presha kuhusu takwimu zake binafsi kwa sababu jambo muhimu ni timu yake kuendelea kushinda.

“Kila mashindano huwa tofauti. Sina wasiwasi kwa sababu nimefunga bao moja tu. Tunashinda, na hilo ndilo muhimu zaidi,” alisema.

Hispania itakutana na Ufaransa jijini Dallas katika pambano la kutafuta nafasi ya kufuzu kucheza fainali ya Kombe la Dunia, huku Yamal akiwa mmoja wa wachezaji wanaotarajiwa kuamua hatima ya mchezo huo.

Leave a Comment