×

Trump Atoa Nyaraka za Siri, Aishutumu China Kuingilia Uchaguzi wa Marekani 2020

Rais wa Marekani Donald Trump.

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuondoa usiri wa nyaraka anazodai zinaonyesha kuwa China iliingilia uchaguzi wa urais wa mwaka 2020, hatua inayokwenda kinyume na tathmini rasmi ya jumuiya ya ujasusi ya Marekani iliyohitimisha kuwa hakuna ushahidi wa Beijing kuathiri matokeo ya uchaguzi huo.

Akilihutubia taifa kwa dakika 25 kutoka Ikulu ya White House, Trump alisema nyaraka hizo zinaonyesha udhaifu wa kutisha katika mfumo wa uchaguzi wa Marekani na kudai kuwa China ilipata taarifa za wapigakura zaidi ya milioni 220, zikiwemo majina, anuani na taarifa nyingine.

Trump pia alidai baadhi ya maafisa wa jumuiya ya ujasusi walificha taarifa kuhusu kiwango cha shughuli za China zinazohusiana na uchaguzi wa Marekani.

Hata hivyo, tathmini ya mwaka 2021 iliyotolewa na jumuiya ya ujasusi ya Marekani ilibaini kuwa hakuna ushahidi kwamba nchi yoyote ya kigeni ilibadilisha mfumo wa kiufundi wa uchaguzi wa 2020, ikiwemo usajili wa wapigakura, kura, mfumo wa kuhesabu kura au matokeo ya uchaguzi.

Ripoti hiyo, ambayo iliandaliwa wakati John Ratcliffe akiwa Mkurugenzi wa Ujasusi wa Taifa na ambaye sasa ni Mkurugenzi wa CIA, ilieleza kuwa China imekuwa ikikusanya taarifa za wapigakura wa Marekani tangu angalau mwaka 2008 kwa lengo la kuchambua maoni ya umma na kutabiri matokeo ya uchaguzi, lakini si kuathiri moja kwa moja mchakato wa uchaguzi.

Kwa mujibu wa watu wawili wanaofahamu suala hilo, taarifa za wapigakura zilizokusanywa na China hazikuwa za siri kwani kwa kawaida hupatikana kwa njia halali na hutumiwa na washauri wa kisiasa, hivyo hazingeweza kutumika kubadilisha matokeo ya uchaguzi.

Hotuba ya Trump imekuja wakati Chama cha Republican kinakabiliwa na mazingira magumu kisiasa kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula (midterm elections), huku umaarufu wa rais ukipungua kutokana na vita dhidi ya Iran na kupanda kwa bei za nishati.

Trump pia ametumia fursa hiyo kuwataka wabunge wa Republican kupitisha sheria mpya zinazohitaji kitambulisho cha mpigakura na uthibitisho wa uraia kabla ya kupiga kura, ingawa wapinzani wake wa Democratic wameendelea kupinga mapendekezo hayo.

Wakati huo huo, ubalozi wa China nchini Marekani umekanusha madai hayo, ukisisitiza kuwa China haijawahi na haitawahi kuingilia uchaguzi wa rais wa Marekani.

Leave a Comment