×

Mwigizaji wa Godzilla vs. Kong, Kaylee Hottle, Afariki Akiwa na Miaka 18

Mwigizaji chipukizi Kaylee Hottle, aliyefahamika kwa kuigiza nafasi ya Jia katika filamu za Godzilla vs. Kong (2021) na Godzilla x Kong: The New Empire (2024), amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 18.

Kwa mujibu wa baba yake, Joshua Hottle, Kaylee alipoteza maisha baada ya kuhusika katika ajali ya gari iliyotokea asubuhi ya Julai 21, 2026, huko Maryland, Marekani. Alieleza kuwa binti yake alifariki akiwa njiani kupelekwa hospitalini.

Mwigizaji chipukizi Kaylee Hottle, aliyefahamika kwa kuigiza nafasi ya Jia katika filamu za Godzilla vs. Kong (2021) .

Joshua alithibitisha taarifa hizo kupitia video aliyoshiriki kwenye Facebook kwa kutumia Lugha ya Alama ya Marekani (ASL), huku akieleza kuwa alikuwa akisafiri kutoka Texas kwenda Maryland kwa ajili ya kuchukua mwili wa binti yake.

Kaylee na wazazi wake wote walikuwa watu wenye uziwi, na alisoma katika Texas School for the Deaf. Shule hiyo ilitoa salamu za rambirambi, ikimtaja Kaylee kuwa mwanafunzi aliyependwa na mwenye kipaji kikubwa.

Safari yake ya uigizaji ilianza mwaka 2017 baada ya kuonekana kwenye tangazo la programu ya kutafsiri Lugha ya Alama (Convo). Tangazo hilo lilimfanya atambuliwe na watayarishaji wa filamu ya Godzilla vs. Kong, ambao walimchagua kuigiza nafasi ya Jia, msichana yatima anayejenga uhusiano wa kipekee na King Kong kupitia Lugha ya Alama.

Mbali na filamu hizo, Kaylee aliigiza pia katika kipindi cha televisheni Magnum P.I. mwaka 2021. Mwaka 2024 alipata uteuzi wa Saturn Awards katika kipengele cha Best Younger Performer in a Film kutokana na uigizaji wake katika Godzilla x Kong: The New Empire.

Kaylee Hottle, Marchi 25, 2024.

Muigizaji mwenzake, Alexander Skarsgård, aliwahi kumsifu Kaylee kwa weledi wake mbele ya kamera, akisema licha ya kuwa ilikuwa filamu yake ya kwanza, alikuwa na uwezo mkubwa wa kuelewa maelekezo na kuigiza kwa ustadi wa hali ya juu.

Kifo chake kimeacha simanzi kubwa kwa familia, mashabiki na wadau wa tasnia ya filamu duniani.

Leave a Comment