
Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mchungaji Peter Msigwa, leo Julai 22, 2026, alifika katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, kufuatilia shauri la kikatiba lililofunguliwa na mawakili wa Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu.
Shauri hilo, ambalo limesajiliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu ya Dodoma, linahusu malalamiko ya mawakili hao wakidai kunyimwa haki ya kuonana na mteja wao gerezani kwa faragha, pamoja na kuwepo kwa mazingira yasiyoruhusu mawasiliano ya siri wanapokwenda kumwona.
Baada ya kesi hiyo kuahirishwa kwa muda, Mchungaji Msigwa alipata nafasi ya kukutana na viongozi na wanachama wa CHADEMA waliokuwa wamefika mahakamani kufuatilia mwenendo wa shauri hilo, ambapo walionekana wakisalimiana na kukumbatiana nje ya mahakama.
Shauri hilo linaendelea kufuatiliwa kwa karibu kutokana na umuhimu wake katika masuala ya haki za mawakili na faragha ya mawasiliano kati ya wakili na mteja.

