×

Waziri Mkuu Ataka Uwajibikaji katika Matumizi ya Fedha za NBC Marathon

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba.

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amezitaka wizara na taasisi zinazonufaika na fedha zinazopatikana kupitia NBC Dodoma Marathon kuhakikisha zinatumia fedha hizo kwa uwazi, uwajibikaji na kuzingatia thamani ya fedha ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa na kuleta matokeo yanayopimika.

Akizungumza Julai 26, 2026, wakati wa uzinduzi wa msimu wa saba wa NBC Dodoma Marathon uliofanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Dkt. Nchemba alisema kila shilingi inayowekezwa kupitia mbio hizo inapaswa kuleta matokeo yanayoonekana, hususan katika kuboresha huduma za afya kwa Watanzania.

Alisema NBC Dodoma Marathon imekua na kuvuka mipaka ya kuwa mashindano ya riadha pekee, na sasa ni jukwaa muhimu la kuhamasisha afya, kuimarisha ustawi wa jamii, kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na kuchangia uboreshaji wa huduma za afya nchini.

Uzinduzi huo ulifanyika chini ya kaulimbiu ya #KataWeseOkoaMaisha, ambapo Waziri Mkuu aliipongeza Benki ya NBC, wadhamini na washiriki wote kwa mchango wao katika kufanikisha tukio hilo na kusaidia juhudi za kuboresha afya za Watanzania.

“Napenda kuwapongeza waandaaji wa NBC, wadhamini na washiriki wote. Hili si tukio la michezo pekee, bali ni jukwaa la kufadhili na kuimarisha ustawi wa jamii,” alisema.

Aidha, Dkt. Nchemba alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya afya na kuimarisha huduma za matibabu, akieleza kuwa afya bora ndiyo msingi wa maendeleo ya mtu binafsi na Taifa kwa ujumla.

“Afya ni msingi wa maendeleo. Ukiwa na afya njema unaweza kushiriki shughuli za uzalishaji na hata mashindano kama haya ya marathon. Serikali itaendelea kuhakikisha jitihada hizi zinakuwa endelevu,” alisisitiza.

Leave a Comment