×

Wanawake 40 Kupata Mafunzo na Mashine za Kushona kupitia Ufadhili Mpya

Standard Chartered Foundation kupitia Standard Chartered Tanzania imetoa msaada wa Sh21.46 milioni kwa ajili ya kuunga mkono Programu ya Mabinti ya CCBRT, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha wanawake walio katika mazingira magumu kujitegemea kiuchumi.

Fedha hizo zitatumika kugharamia mafunzo ya wiki sita kwa wanawake 40 katika ushonaji, utengenezaji wa bidhaa za crochet, urembaji wa nguo (embroidery), usimamizi wa biashara na elimu ya fedha. Pia zitanunua mashine za kushona zitakazowasaidia wanufaika kuanzisha au kupanua shughuli za kujipatia kipato.

Programu ya Mabinti ya CCBRT inawalenga wanawake wenye ulemavu, manusura wa fistula ya uzazi, wasichana walioacha shule na wanawake wanaokabiliwa na changamoto za kiuchumi na kijamii. Kupitia mafunzo ya ujuzi na ujasiriamali, programu hiyo inalenga kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kuboresha maisha yao.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Standard Chartered Tanzania, Geofrey Mchangila, alisema msaada huo unaendeleza ushirikiano kati ya benki hiyo na CCBRT katika kuwawezesha wanawake kwa kuwapatia mafunzo ya stadi za kazi, elimu ya fedha na vifaa vitakavyowawezesha kujitegemea kiuchumi.

Alisema benki hiyo ilianza ushirikiano na CCBRT mapema mwaka huu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake kwa kukabidhi mashine 12 za kushona na kutoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wanufaika wa Programu ya Mabinti.

Mchango huo umetolewa sambamba na maadhimisho ya miaka 20 ya Mpango wa Kujitolea wa Wafanyakazi wa Standard Chartered, ambao umeendelea kuhamasisha wafanyakazi kutumia muda, ujuzi na uzoefu wao kuchangia maendeleo ya jamii.

Leave a Comment