×

Iran Yafichua Sababu ya Kutotoa Sauti ya Kiongozi Mpya Mojtaba Khamenei

Kiongozi mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mojtaba Khamenei.

Gazeti la Hamshahri, linalomilikiwa na Manispaa ya Tehran, limedai kuwa sababu ya kutotolewa kwa sauti ya Kiongozi mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mojtaba Khamenei, ni hofu ya uwezekano wa teknolojia za kisasa kutumiwa na mashirika ya kijasusi kubaini mahali alipo.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, rekodi za sauti zinaweza kuwa chanzo cha taarifa nyeti, kwani mwangwi (echo) unaopatikana kwenye sauti unaweza kusaidia kubaini chumba au eneo ilikorekodiwa.

Hamshahri pia limedai kuwa wataalamu wa kijasusi wana uwezo wa kuchambua mabadiliko madogo ya mfumo wa umeme yanayojitokeza kwenye rekodi za sauti na kuyatumia kubaini nchi, tarehe, muda na hata eneo halisi ambako rekodi ilifanyika.

Aidha, gazeti hilo limesema kifaa kilichotumika kurekodi sauti nacho kinaweza kutoa taarifa muhimu, kwa kuwa kila simu au kifaa cha kurekodi huwa na sifa za kipekee zinazoweza kutumika kukitambua, sawa na alama za vidole.

Vilevile, sauti za mazingira kama upepo, ndege, wadudu, magari au mifumo ya uingizaji hewa zinaweza kuchunguzwa na kusaidia kubaini eneo la kijiografia alikokuwa mtu aliyerekodiwa.

Tangu Mojtaba Khamenei ateuliwe kuwa kiongozi wa tatu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hajawahi kuonekana hadharani, wala picha au rekodi ya sauti yake haijatolewa rasmi. Vyombo vya habari vya Iran vimeendelea kuchapisha ujumbe wa maandishi unaodaiwa kutoka kwake, jambo lililozua mjadala kuhusu hatua hiyo ya usiri.

Leave a Comment