
Dodoma. Kampuni ya mawasiliano ya Yas imewahimiza wakulima nchini kutumia huduma za kidijitali kupata taarifa muhimu kuhusu masoko, hali ya hewa na fursa za biashara, hatua inayoweza kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi na kuongeza tija katika shughuli zao za kilimo.
Akizungumza wakati wa Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Kaimu Mkuu wa Yas Kanda ya Kati, Richard Mmari, amesema maendeleo ya teknolojia na upanuzi wa huduma za mawasiliano nchini yamefungua fursa kubwa kwa wakulima kutumia simu na huduma za kidijitali katika hatua mbalimbali za uzalishaji.
Mmari amesema mkulima wa sasa anaweza kupata taarifa muhimu akiwa shambani au nyumbani, ikiwemo bei za mazao katika masoko, utabiri wa hali ya hewa na taarifa kuhusu fursa mbalimbali za kibiashara.
“Leo mkulima anaweza kutumia simu kupata taarifa za bei za mazao, kufuatilia hali ya hewa na kutafuta masoko akiwa shambani au nyumbani. Hizi ni fursa ambazo zinaweza kumsaidia kupanga vizuri shughuli zake na kuongeza tija,” amesema Mmari.
Amesema Yas imewekeza katika zaidi ya minara 4,900 ya 4G na 5G nchini, hatua ambayo imepanua upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa Watanzania wengi, wakiwemo wananchi wanaoishi katika maeneo ya vijijini ambako shughuli za kilimo zinafanyika kwa kiasi kikubwa.
Mbali na upanuzi wa mtandao, Mmari amesema Yas inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wananchi kumiliki vifaa vinavyowawezesha kutumia huduma za kidijitali, ikiwemo simu janja zinazopatikana kupitia mpango wa malipo kwa awamu.
Kwa mujibu wa Mmari, wakulima wanaotembelea Maonesho ya Nanenane jijini Dodoma wanaweza kufika katika banda la Yas kupata maelezo zaidi kuhusu mpango huo pamoja na huduma nyingine za kidijitali zinazoweza kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku.
Yas imesema itaendelea kuboresha na kupanua huduma zake za mawasiliano, hususan katika maeneo ya vijijini, kwa lengo la kuwawezesha wakulima na wananchi wengine kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.