
JOSE Mourinho amefichua kuwa aliwahi kusaini makubaliano ya kuchukua nafasi ya ukocha wa Manchester United kutoka kwa Sir Alex Ferguson mwaka 2013, lakini akabadilisha uamuzi baada ya kutoa ahadi ya kurejea Chelsea.
Mourinho amefichua siri hiyo kupitia makala yake mpya ya Netflix, akieleza kuwa alikubaliana kuichukua Manchester United baada ya kuondoka Real Madrid.
“Nilikwenda Chelsea mwaka 2013, lakini katika kipindi hicho kuna jambo ambalo hakuna anayelijua. Nilipoondoka Real Madrid, nilisaini na Manchester United ili niende huko baada ya Sir Alex,” alisema Mourinho.
Kocha huyo wa Ureno alisema alivutiwa sana na ukubwa wa Manchester United na aliona kuwa ni moja ya klabu zenye mvuto mkubwa duniani.
“Bila shaka nilifurahishwa sana, kwa sababu Manchester United ina mvuto wa kipekee. Ninaposema Real Madrid ndiyo klabu kubwa zaidi duniani, lazima niseme Manchester United iko karibu sana,” alisema.
Sir Alex Ferguson pia anaonekana kwenye makala hiyo na kueleza namna Mourinho alivyomjulisha kuwa angechukua nafasi yake, kabla ya simu moja kubadilisha kila kitu.
Ferguson alisema Mourinho alimpigia simu jioni na alikuwa akilia, akimweleza kuwa hawezi kuchukua nafasi hiyo kwa sababu tayari alikuwa ametoa ahadi kwa Chelsea.
“Alinipigia simu mapema jioni akiwa analia. Akasema, ‘Alex, siwezi kufanya hivyo – nimetoa neno langu kwa Chelsea na sitavunja ahadi yangu.’ Sababu aliyotoa niliweza kuielewa, lakini nilikatishwa tamaa,” alisema Ferguson.
Hatimaye, Mourinho alirejea Chelsea kwa kipindi chake cha pili mwaka 2013, wakati Ferguson alistaafu mwishoni mwa msimu huo na nafasi yake ikachukuliwa na David Moyes.
Mourinho alikuja kuinoa Manchester United mwaka 2016akichukua nafasi ya Louis van Gaal. Katika kipindi chake cha takribani miaka miwili na nusu Old Trafford, Mourinho aliisaidia Manchester United kushinda UEFA Europa League, Carabao Cup na Community Shield.
Hatua hiyo inaifanya siri hiyo ya mwaka 2013 kuwa moja ya matukio ambayo yangeweza kubadilisha kabisa historia ya Manchester United baada ya enzi ya Sir Alex Ferguson.