
Bilionea na mwanzilishi wa Amazon, Jeff Bezos, amekumbana na ukosoaji baada ya kutangaza ahadi ya kuchangia dola milioni 200 (Shilingi bilioni 529) kwa ajili ya kulinda wanyama 100 walio katika hatari kubwa zaidi ya kutoweka duniani.
Mpango huo unaojulikana kama Phoenix Species Project, umeanzishwa kwa ushirikiano na mwigizaji wa Hollywood Leonardo DiCaprio, ambaye alitangaza mpango huo kupitia ukurasa wake wa Instagram.
DiCaprio amesema mpango huo ni moja ya juhudi kubwa zaidi za kibinafsi kuwahi kufanyika kwa ajili ya kuokoa viumbe walio katika hatari kubwa ya kutoweka, huku ukilenga miradi katika takribani nchi 30.
“Hatuokoi viumbe hawa pekee, bali tunalinda kila kitu kinachowazunguka; misitu, mito,” amesema DiCaprio.
Hata hivyo, badala ya kupongeza hatua hiyo, baadhi ya watu wamemshambulia Bezos wakidai kuwa mchango huo ni aina ya ‘greenwashing’, yaani matajiri au makampuni makubwa kutumia misaada ya mazingira kujenga taswira nzuri huku wakikabiliwa na lawama kutokana na athari kubwa wanazozalisha kwa mazingira.
Baadhi ya wakosoaji kwenye mitandao ya kijamii wamehoji kwa nini watu wenye utajiri mkubwa wanatoa fedha kusaidia kutatua matatizo ya mazingira ambayo, kwa kiasi fulani, wanadaiwa kuchangia kuyasababisha.
Ukosoaji huo unakuja wakati Bezos akiwa tayari amewahi kukabiliwa na tuhuma za aina hiyo. Mwaka 2020, Bezos Earth Fund ilitangaza mpango wa kutoa dola bilioni 10 sawa na TSh trilioni 26 kwa ajili ya kulinda mazingira na viumbe hai pamoja na kusaidia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Wakosoaji pia wameelekeza kidole kwa Amazon, wakidai kampuni hiyo imekuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa hewa ukaa. Kwa mujibu wa taarifa zilizotajwa katika habari hiyo, uzalishaji wa hewa ya ukaa wa Amazon uliongezeka kwa asilimia 18 kati ya mwaka 2020 na 2021.
Aidha, kampuni ya Bezos ya anga za juu, Blue Origin, nayo imeibua mijadala kuhusu athari za shughuli zake kwa mazingira.
Kwa ujumla, mjadala unaendelea kugawanyika kati ya wanaoona mchango wa bilioni 529 kama hatua muhimu ya kuokoa viumbe vilivyo hatarini na wale wanaoamini kuwa juhudi hizo hazitoshi kuondoa madhara ya kimazingira yanayohusishwa na shughuli za kibiashara za Bezos.