
Washington, Marekani — Agosti 11, 2026: Rais wa Marekani, Donald Trump, alihamishwa kwa siri kutoka kwenye ndege yake ya Air Force One kupitia gari la huduma za chakula (catering truck) na kupandishwa kwenye ndege nyingine ndogo, baada ya kupatikana kwa tishio la kujaribiwa kuuawa na Iran, kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Marekani.
Kwa mujibu wa Washington Post, tukio hilo lilitokea mwezi uliopita baada ya Trump kuhudhuria mkutano wa NATO nchini Uturuki. Awali Ikulu ya Marekani ilisema Trump angeondoka Uturuki kwa kutumia Air Force One kuelekea Uingereza.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya Trump kupanda ndege hiyo mbele ya kamera, alishushwa kwa siri kupitia gari la kubeba chakula na kupelekwa kwenye ndege aina ya Air Force C-32A, iliyokuwa ikisubiri katika eneo la uwanja wa ndege.
Ndege ya zamani ya Air Force One iliendelea safari ikiwa kama kivuli (decoy), huku baadhi ya waandishi wa habari na hata baadhi ya wafanyakazi wa Ikulu wakiamini kuwa Trump alikuwa ndani yake.
TISHIO LA IRAN LILISABABISHA OPARESHENI HIYO
Washington Post imesema operesheni hiyo ilianzishwa baada ya mamlaka za Marekani kupata taarifa kuhusu tishio linaloaminika dhidi ya maisha ya Trump.
Hali hiyo ilitokea wakati mvutano na uhasama kati ya Marekani na Iran ukiwa umeongezeka, huku Iran ikiwa inapakana na Uturuki.
Waandishi wa habari waliokuwa wakisafiri kwenye Air Force One ya zamani waliambiwa kufunga mapazia ya madirisha katika sehemu yao. Baadaye Trump alipoulizwa kwa nini waliambiwa kufanya hivyo, alijibu kwa mzaha kwamba huenda walikuwa kwenye “safari hatari.”
Ndege ya C-32A iliyokuwa imembeba Trump ilifika Uingereza karibu saa 4:20 usiku, huku Air Force One ya zamani pamoja na waandishi wa habari ikifika dakika chache baadaye.
Haijafahamika wazi Trump alihamishwa vipi kutoka C-32A na kurejea kwenye Air Force One ya zamani kabla ya kuonekana akishuka kwenye ndege hiyo.
IKULU YATHIBITISHA KUWEPO KWA VITISHO
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Steve Cheung, alisema ndege mpya iliyotolewa na Qatar imewekewa mifumo ya juu ya kiusalama inayolenga kuhakikisha usalama wa rais na wafanyakazi wake.
Alisema kuna “maadui wengi wa Marekani” wanaomlenga Trump na kwamba serikali inatumia kila njia iliyopo kukabiliana na vitisho hivyo.
Ndege hiyo mpya ni Boeing 747 iliyotolewa na Qatar kwa Marekani na baadaye kufanyiwa maboresho na kampuni ya ulinzi ya L3Harris Technologies. Ilitarajiwa kutumika kwa muda kama mbadala wa Air Force One wakati Boeing ikichelewa kukamilisha ndege mpya za rais wa Marekani.
