
Msanii maarufu wa muziki na mfanyabiashara wa urembo, Rihanna, ameshiriki picha adimu akiwa pamoja na watoto wake wote watatu alipowapeleka katika nyumba na mtaa aliokulia huko Bridgetown, Barbados.
Rihanna, ambaye amekuwa akilinda sana maisha binafsi ya watoto wake, aliweka picha hizo kwenye Instagram akiwa pamoja na wanawe wawili, RZA (4) na Riot (2), pamoja na binti yake Rocki Irish, mwenye miezi 10. Watoto hao ni wa Rihanna na mwanamuziki A$AP Rocky.
Katika ujumbe wake, Rihanna alieleza kwa hisia namna maisha yake yalivyobadilika kutoka kuwa mtoto aliyekulia eneo hilo hadi sasa kurudi akiwa na watoto wake mwenyewe.

Mtaa huo, ambao zamani uliitwa Westbury New Road, ulipewa jina Rihanna Drive mwaka 2017 kwa heshima ya msanii huyo na baadaye kutambuliwa kama alama muhimu ya utamaduni katika eneo hilo.
Rihanna kwa sasa anatumia muda na familia yake nchini Barbados. Mapema mwezi huu alionekana kwenye Grand Kadooment Day Parade, tukio kubwa linalofunga sherehe za Crop Over Festival, akiwa amevalia vazi la kuvutia lililopambwa kwa vito na mapambo ya manyoya.
Akizungumza hapo awali kuhusu uhusiano wake na Barbados, Rihanna alisema nchi hiyo imekuwa sehemu ya maisha na kazi zake, akisisitiza kuwa urithi wake wa Barbados utaendelea kuonekana katika mambo anayofanya.

Inaonekana sasa anataka kuhakikisha urithi huo unakuwa sehemu pia ya maisha ya watoto wake.
Rihanna na A$AP Rocky wamekuwa kwenye uhusiano tangu mwaka 2020 na kwa pamoja wana watoto watatu. Rocky, ambaye jina lake halisi ni Rakim Athelaston Mayers, pia ana uhusiano wa karibu na Barbados kupitia marehemu baba yake, ambaye alikuwa anatoka nchini humo.
Kwa Rihanna, ziara hiyo haikuwa tu kumbukumbu ya maisha yake ya utotoni, bali pia ilikuwa fursa ya kuwarudisha watoto wake kwenye mizizi ya mama yao.