×

Presha ya Mashabiki Yamfanya Cardi B Kutaka Kupumzika

Rapa maarufu wa Marekani, Cardi B, amezua gumzo baada ya kusema anataka kuchukua mapumziko ya muda kwenye muziki kutokana na presha anayopata kutoka kwa mashabiki kuhusu kasi ya kutoa nyimbo na video.

Cardi B ametoa kauli hiyo Alhamisi, Agosti 13, 2026, wakati akizungumza na mashabiki kupitia X Spaces, ambapo ameeleza kuwa malalamiko kuhusu ratiba yake ya muziki hayamsukumi kufanya kazi zaidi, bali yanamfanya azidi kutamani kupumzika.

Rapa huyo amesema tayari alikuwa amepanga kutumia kipindi hiki cha kiangazi kupunguza shughuli za muziki na kutumia muda zaidi na familia yake, badala ya kutumia muda mwingi studio.

Kauli hiyo imekuja wakati baadhi ya mashabiki wakimshinikiza kutoa muziki na video kwa kasi zaidi, huku wengine wakitaka baadhi ya nyimbo zake ziambatane na video kubwa pamoja na kampeni za matangazo.

Hata hivyo, Cardi B ameonekana kutokubaliana na mtazamo huo, akisisitiza kuwa si kila wimbo anaoutoa lazima uambatane na video kubwa au kampeni kubwa ya matangazo.

Kauli hiyo imeibua mjadala miongoni mwa mashabiki wake, huku baadhi wakimuunga mkono na kusema msanii anapaswa kuwa na uhuru wa kuamua ratiba yake ya kazi, wakati wengine wakisubiri kuona iwapo kweli atapunguza shughuli zake za muziki.

Cardi B, mwenye jina halisi la Belcalis Marlenis Almánzar, alizaliwa Oktoba 11, 1992, jijini New York, Marekani. Amejijengea jina kubwa katika muziki wa hip-hop na kuwa miongoni mwa marapa wanawake wenye ushawishi mkubwa duniani.

Ingawa bado anaendelea na shughuli zake za muziki, kauli yake ya hivi karibuni imewaacha mashabiki wakijiuliza iwapo atachukua mapumziko rasmi au ataendelea kutoa kazi mpya kwa ratiba atakayoichagua mwenyewe.

Na Razaku Ramadhan | GPL

Leave a Comment