×

TEC Yafunguka Kuhusu Kikao na Rais Samia, Yatoa Ushauri wa Kuponya Nchi – Video

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limesema lengo kuu la kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, lilikuwa kumshirikisha mtazamo wao kuhusu hali ya kisiasa nchini na kutoa ushauri wa namna Tanzania inaweza kurejesha utulivu na kuponya majeraha yaliyotokana na matukio ya Uchaguzi Mkuu uliopita.

Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 13, 2026, kufuatia kikao kilichofanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma Agosti 10, Katibu Mkuu wa TEC, Padre Dkt. Charles Kitima, amesema mkutano huo ulitokana na ombi la maaskofu wenyewe waliotaka kumfikishia Rais maoni yao kuhusu hali ya nchi.

Padre Kitima amesema maaskofu walimkabidhi Rais Samia andiko rasmi lenye kurasa nne, likieleza hatua wanazoona ni muhimu kuchukuliwa ili kurejesha utulivu na kujenga upya mahusiano kati ya serikali na wananchi.

Kwa mujibu wa Padre Kitima, msingi mkubwa wa ujumbe wao ni kusimamia ukweli, kusameheana na hatimaye kuifikisha nchi katika hatua ya uponyaji.

“To admit the truth, then reconciliation, healing the nation,” alisema Padre Kitima, akieleza msimamo wa maaskofu kuhusu mchakato huo.

Amesema viongozi wa kiroho wanaona umuhimu wa kuwa na ujasiri wa kutaja mambo yaliyokwenda mrama ili kuwezesha mchakato wa maridhiano kuwa na matokeo yenye maana.

Padre Kitima amesisitiza kuwa bila kukiri ukweli kuhusu yaliyotokea, juhudi za maridhiano zinaweza kukosa msingi wa kutosha wa kurejesha uaminifu uliopotea kati ya wananchi na mamlaka.

Aidha, Katibu Mkuu huyo amesema matukio ya Oktoba 29, 2025 yameacha maumivu na sononeko kwa Watanzania wengi, huku yakichangia kupungua kwa imani ya baadhi ya wananchi kwa mamlaka zao.

Amesema TEC imeeleza masikitiko yake kuhusu mauaji na uharibifu wa mali uliotokea, huku ikisisitiza umuhimu wa kushughulikia sababu zilizopelekea watu kuingia katika maandamano na hali ya mvutano wa kisiasa.

Padre Kitima amewataka Watanzania kuwa na utulivu na kuendelea kuwa na imani katika mchakato wa kutafuta suluhisho la changamoto zilizopo.

Kwa upande wa TEC, uponyaji wa taifa hauwezi kupatikana kwa kupuuza yaliyopita, bali unahitaji ukweli, msamaha, kusameheana na kujenga upya mahusiano yaliyovunjika.

Mkutano huo kati ya TEC na Rais Samia unakuja wakati Tanzania ikiendelea na mjadala mpana kuhusu hali ya kisiasa nchini na namna ya kujenga maridhiano na utulivu baada ya matukio yaliyotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita.

Leave a Comment