×

Arsenal na Manchester City Kukiwasha Mechi ya Ngao ya Jamii leo

CARDIFF, Wales — Arsenal itaanza rasmi msimu wa 2026/27 kwa mtihani mkubwa dhidi ya Manchester City katika mchezo wa Community Shield (Ngao ya Jamii) utakaochezwa leo Jumapili Agosti 16, 2026 saa kumi na mija jioni kwenye Uwanja wa Principality Stadium, Cardiff.

Mchezo huo unawakutanisha miamba hiyo ya soka la England katika mchezo wa jadi unaofungua msimu, huku kila timu ikiwa na changamoto zake za kikosi baada ya mapumziko ya Kombe la Dunia.

Arsenal wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na wasiwasi upande wa ulinzi. Beki William Saliba bado anasumbuliwa na jeraha la mgongo, wakati Jurrien Timber anaendelea kupona jeraha la kinena.

Kutokana na hali hiyo, Cristhian Mosquera anatarajiwa kuungana na Gabriel katikati ya ulinzi, huku Ben White na Riccardo Calafiori wakitarajiwa kucheza pembeni.

Hata hivyo, Arsenal wamepata taarifa nzuri kuhusu Bukayo Saka, Declan Rice na David Raya, ambao wamerudi mazoezini baada ya mapumziko yao kufuatia Kombe la Dunia.

Raya alishapata nafasi ya kucheza katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Como, hivyo ana nafasi kubwa ya kuanza dhidi ya City. Saka na Rice nao wanatarajiwa kucheza, lakini kuna uwezekano mkubwa wakaanzia benchi kutokana na kutoshiriki maandalizi yote ya msimu.

Macho pia yatakuwa kwa Bruno Guimaraes, ambaye anaweza kuanza mchezo wake wa kwanza wa ushindani akiwa na Arsenal. Kiungo huyo wa Brazil anatarajiwa kucheza pamoja na Myles Lewis-Skelly na nahodha Martin Odegaard.

Kwa upande wa Manchester City, changamoto kubwa ni kutokuwepo kwa kiungo wao muhimu Rodri, ambaye bado yupo nje baada ya kufanyiwa upasuaji wa mgongo.

Erling Haaland na Elliot Anderson pia wameanza mazoezi hivi karibuni baada ya mapumziko ya Kombe la Dunia, hivyo huenda wakaanzia benchi.

City wanatarajiwa kutegemea uwezo wa Phil Foden, Antoine Semenyo na Omar Marmoush katika safu ya ushambuliaji.

Kukosekana kwa Rodri kunaweza kuwa na athari kubwa kwa City, hasa katika udhibiti wa mchezo na kumiliki mpira. Arsenal, kupitia Guimaraes, Odegaard na Lewis-Skelly, watakuwa na nafasi ya kujaribu kuvunja presha ya City na kutawala eneo la kiungo.

Upande wa Arsenal pia utakuwa muhimu katika mchezo huo, huku ushirikiano wa Odegaard, White na Max Dowman ukitarajiwa kuwa silaha mojawapo ya kuwavuruga mabeki wa City.

Kwa ujumla, timu zote zinaingia kwenye mchezo huo bila kuwa na vikosi kamili, jambo linalofanya matokeo kuwa magumu kutabirika.

Arsenal wanaonekana kuwa na nguvu zaidi kwenye kiungo, lakini majeraha ya Saliba na Timber pamoja na kurejea kwa kuchelewa kwa Saka na Rice yanaweza kuwaathiri.

City nao watakabiliwa na pengo kubwa la Rodri, mchezaji ambaye amekuwa muhimu katika kuwapa udhibiti wa michezo.

Ikiwa mchezo huo utaisha kwa sare baada ya dakika 90, mshindi ataamuliwa kwa mikwaju ya penalti, hivyo kuongeza mvuto wa pambano hilo la ufunguzi wa msimu.

Leave a Comment