×

The Africa Rally Yachangisha Milioni 20 kwa Chuo cha Ufundi cha Safal ALAF

Taasisi ya Safal ALAF Foundation imepokea takribani shilingi milioni 20 zilizopatikana kupitia safari maalumu ya magari ya zamani inayojulikana kama The Africa Rally, iliyofanyika mwaka huu kutoka Hartbeespoort nchini Afrika Kusini hadi Bagamoyo, Tanzania.

Safari hiyo yenye urefu wa kilomita 6,000 ilihusisha washiriki 50 waliovuka nchi tano kwa kutumia magari ya kizamani, kabla ya kuhitimisha safari yao mjini Bagamoyo.

Fedha hizo zitatumika kununua vifaa kwa ajili ya Safal ALAF Technical Training Institute iliyopo Arusha, kupitia kampeni ya Miles for Education, inayolenga kuwawezesha vijana kupata mafunzo ya vitendo na ujuzi wa ufundi, pamoja na fursa za kujiajiri na kuajiriwa.

Akizungumza kuhusu safari hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa ALAF Limited, Hawa Bayumi, aliwapongeza washiriki kwa kufanikisha safari hiyo, akisema jitihada zao zitasaidia kukuza ujuzi wa kiufundi na kuongeza fursa kwa vijana watakaopata nafasi ya kusoma katika taasisi hiyo.
“Kila maili katika safari hii ya kilomita 6,000 ilikuwa ni ishara ya kujituma, uthabiti na hatua nzuri kuelekea kupata matokeo yenye manufaa,” alisema Bayumi.

Kwa upande wake, Sangeet Shah, aliyeliwakilisha ALAF katika safari hiyo pamoja na dereva mwenzake Tim Pick, alisema walifurahia kushiriki katika tukio hilo kwa sababu lengo lake lilikuwa kuchangisha fedha kwa ajili ya taasisi hiyo.

Shah na Pick walitumia gari aina ya Mercedes-Benz ya zamani katika safari hiyo, huku Shah akisema kukamilisha safari hiyo kulikuwa mafanikio makubwa kwao na kwa vijana watakaonufaika na chuo hicho.
“Lengo kuu lilikuwa ni kuchangia katika ujenzi wa Safal ALAF Technical Institute na tunafurahi kuwa tumeweza kukamilisha safari hii kikamilifu na kutimiza malengo, kwani taasisi hii itawasaidia vijana wengi kutimiza malengo yao,” alisema Shah.

Naye muandaaji wa The Africa Rally, Paul Clayton, alisema zaidi ya Randi milioni 1.1, sawa na takribani shilingi milioni 173 za Tanzania, zimekusanywa kupitia tukio hilo na zitatumika katika miradi mbalimbali.

Clayton alisema chuo cha ufundi cha ALAF kitapokea takribani Randi 119,000, sawa na shilingi milioni 20 za Tanzania, huku akibainisha kuwa kiasi hicho kinaweza kuongezeka kwa kuwa zoezi la kuchangia bado linaendelea.

Aliwataka watu wanaopenda kuunga mkono mpango huo kuendelea kuchangia kupitia jukwaa la The Africa Rally ili kusaidia juhudi za kuendeleza taasisi hiyo ya mafunzo ya ufundi.

Kwa upande wake, Pick alisema safari hiyo imewapa uzoefu mkubwa, hasa kutokana na kushiriki katika tukio lililokuwa na lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwawezesha vijana kupata elimu na ujuzi wa ufundi.

The Africa Rally imekuwa ikiandaliwa kwa miaka kadhaa, huku safari ya mwaka huu ikihitimishwa Bagamoyo baada ya washiriki kukatiza katika nchi tano. Waandaaji pia wameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Bodi ya Utalii Tanzania kwa ushirikiano uliotolewa katika kufanikisha safari hiyo.

Leave a Comment