
Dar es Salaam, 20 Agosti 2026: Vodacom Tanzania Plc imeendelea kuonyesha ukuaji imara na kuzalisha thamani kwa wanahisa, wateja na jamii katika mwaka wa fedha uliomalizika Machi 31, 2026, mafanikio yaliyochangiwa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji endelevu katika miundombinu ya mawasiliano, huduma za kidijitali na huduma jumuishi za kifedha.
Matokeo haya yamebainishwa leo wakati wa Mkutano Mkuu wa 10 wa Mwaka wa Wanahisa wa Kampuni, ambapo wanahisa walijadili na kuidhinisha maazimio muhimu yanayohusiana na utendaji wa Kampuni kwa mwaka wa fedha 2026, malipo ya gawio, muundo wa Bodi, utawala bora pamoja na mwelekeo wa biashara kwa siku zijazo.
Katika mwaka wa fedha 2026, mapato ya huduma yaliongezeka kwa asilimia 21.8 hadi kufikia Shilingi trilioni 1.8, wakati faida kabla ya kutoa gharama za riba, kodi, uchakavu na upunguzaji thamani (EBITDA) iliongezeka kwa asilimia 38.8 hadi kufikia Shilingi bilioni 684.9.
Faida baada ya kodi iliongezeka kwa asilimia 18.4 hadi Shilingi bilioni 107.1, huku ukuaji wa faida halisi baada ya kodi ukifikia asilimia 125.5. Aidha Kampuni pia iliongeza idadi ya wateja wake hadi milioni 27.7, sawa na ongezeko la asilimia 22.3, ikichagizwa na ongezeko la asilimia 22.5 la wateja wa intaneti na asilimia 22.6 la wateja wa M-Pesa.
Matokeo haya yalitokana na uwekezaji mkubwa katika mtandao na majukwaa ya kidijitali ya Kampuni. Uwekezaji wa mitaji uliongezeka kwa asilimia 85.1 hadi kufikia Shilingi bilioni 323.9, ukiwezesha kuongezwa kwa vituo vipya 444 vya 4G na 25 vya 5G, sambamba na uwekezaji mkubwa katika mifumo ya TEHAMA na uboreshaji wa mtandao.
Kutokana na uwekezaji huo, wigo wa mtandao wa 4G ulifikia 76.3%, ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.8, huku idadi ya watumiaji wa simu janja ikiongezeka kwa 31.5%. Tangu mwaka 2013, Vodacom Tanzania pia imejenga vituo 466 katika maeneo ya vijijini kupitia mpango wa Serikali wa kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini.
Utendaji huu mzuri wa Kampuni umewezesha pia kuongeza thamani kwa wanahisa. Mkutano Mkuu wa Mwaka umeidhinisha gawio la mwisho la shilingi 23.91 kwa kila hisa ya kawaida kwa mwaka wa fedha 2026, ambalo litalipwa ifikapo au kabla ya tarehe 15 Oktoba 2026 kwa wanahisa waliokuwa kwenye orodha ya wanahisa kufikia mwisho wa biashara tarehe 19 Agosti 2026.
Jumla ya gawio linalopendekezwa kwa mwaka huu wa fedha ni Shilingi bilioni 53.6, sawa na ongezeko la asilimia 18.4 ikilinganishwa na mwaka uliopita, hali inayoakisi sera ya Kampuni kuhusu gawio na dhamira yake ya kuweka uwiano kati ya kutoa thamani endelevu kwa wanahisa na kuendelea kuwekeza katika ukuaji wa biashara.
Mbali na thamani inayotokana moja kwa moja kwa wanahisa, Vodacom Tanzania imeendelea kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi. Katika mwaka wa fedha 2026, Kampuni ilichangia Shilingi bilioni 848 katika mapato ya Serikali kupitia kodi, tozo, ada za masafa ya mawasiliano na ada za udhibiti, huku ikitumia Shilingi bilioni 839 kwa wazabuni na washirika wa ndani wapatao 400. Kampuni pia iliwekeza Shilingi bilioni 6.9 katika mipango ya kijamii na kuwezesha ajira zisizo za moja kwa moja kwa zaidi ya Watanzania 320,000, wakiwemo wafanyakazi huru na mawakala wa M-Pesa.
Akizungumzia utendaji huo, Mkurugenzi wa Fedha wa Vodacom Tanzania Plc, Bi. Hilda Bujiku, alisema:
“Matokeo yetu ya mwaka wa fedha 2026 yanadhihirisha usimamizi makini wa fedha na mtazamo wenye uwiano katika matumizi ya mtaji. Tumeendelea kuimarisha biashara huku tukiwekeza kwa kiasi kikubwa katika mtandao, teknolojia na majukwaa yetu ya kidijitali, na kwa kufanya hivyo, kuzalisha thamani kubwa zaidi kwa wanahisa. Mwelekeo huu unatuweka katika nafasi nzuri ya kuendeleza ukuaji, kudumisha uimara wa kifedha na kunufaika na fursa zijazo katika uchumi wa kidijitali unaoendelea kukua nchini Tanzania.”
Afisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania Plc, Philip Besiimire, alisema:
“Matokeo haya yanaonyesha thamani ya kuwa na mtazamo wa muda mrefu katika uwekezaji na ukuaji. Imani ya wanahisa wetu imetuwezesha kuendelea kuwekeza katika mtandao wetu, teknolojia na huduma za kifedha za kidijitali, huku tukizidi kuboresha utendaji wa biashara na kutoa thamani endelevu kwa wanahisa. Tunapoangalia mbele, tunaendelea kujielekeza katika kujenga biashara imara zaidi, yenye uwezo wa kuhimili changamoto na iliyo tayari kwa siku zijazo, inayozalisha thamani ya kudumu kwa wanahisa, wateja na jamii zetu.”
Mwenyekiti wa Bodi ya Vodacom Tanzania Plc, David Tarimo, alisema:
“Imani na uungwaji mkono unaoendelea kutolewa na wanahisa wetu ni msingi muhimu wa uwezo wetu wa kujenga thamani endelevu kwa muda mrefu. Tutaendelea kujizatiti katika uwekezaji wenye nidhamu, utawala bora na usimamizi wenye uwajibikaji wa mitaji ya wanahisa. Mafanikio yaliyopatikana katika mwaka wa fedha 2026 yanaweka msingi imara wa ukuaji unaoendelea na mchango zaidi katika mustakabali wa uchumi wa kidijitali nchini Tanzania.”
Katika kipindi kijacho, Vodacom Tanzania itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya mtandao, huduma za kifedha za kidijitali, teknolojia, kuboresha uzoefu wa wateja na ubunifu, huku ikiimarisha ushirikiano unaolenga kuchochea maendeleo ya kidijitali na kiuchumi nchini Tanzania.
Kampuni itaendelea kuelekeza uwekezaji wake katika matokeo yanayodumu, kuimarisha utendaji wa biashara, kuboresha huduma kwa wateja, kutoa thamani kwa wanahisa na kuongeza mchango chanya kwa jamii.