×

Ariana Grande Amkosoa Trump, Akataa Muziki Wake Kutumika Kisiasa

Msanii maarufu wa Marekani, Ariana Grande, amemkosoa vikali Rais Donald Trump na timu yake baada ya kutumia wimbo wake “We Can’t Be Friends (Wait for Your Love)” katika video ya TikTok iliyokuwa ikiunga mkono sera za Trump kuhusu watu waliobadili jinsia.

Video hiyo iliyowekwa na akaunti rasmi ya Team Trump Alhamisi, Agosti 20, 2026, ilimuonyesha Trump akielekea kwenye jukwaa la mkutano huku wimbo huo wa Grande ukitumika kama sauti ya video.

Katika video hiyo pia kulikuwa na ujumbe unaosema kuwa wanaume hawawezi kupata watoto na hawapaswi kushindana katika michezo ya wanawake.

Grande, ambaye amekuwa akipinga matumizi ya muziki wake katika kampeni za kisiasa za Trump, alijibu kwenye maoni ya video hiyo akimtaka timu ya Trump kuacha kutumia kazi zake.

“Never use my music again. Also, your truth is false,” aliandika Grande, akimaanisha kuwa muziki wake usitumike tena na pia kupinga ujumbe uliokuwa kwenye video hiyo.

Maoni yake hata hivyo baadaye hayakuonekana tena kwenye chapisho hilo.

Hii si mara ya kwanza kwa Grande kukosoa matumizi ya muziki wake na utawala wa Trump. Juni mwaka huu, White House ilitumia wimbo wake “Bye” katika video iliyohusisha operesheni za Immigration and Customs Enforcement (ICE).

Grande ni miongoni mwa wasanii kadhaa wakubwa ambao wamewahi kupinga matumizi ya nyimbo zao na kampeni au shughuli zinazohusishwa na Trump, wakiwemo Sabrina Carpenter, Katy Perry, SZA, Adele, Rihanna, Céline Dion, Elton John, Neil Young na wengine.

Hatua hiyo inaendelea kuonyesha mvutano kati ya wasanii mbalimbali na timu ya Trump kuhusu matumizi ya muziki wao katika maudhui ya kisiasa bila ridhaa yao.

Leave a Comment