×

Binti wa Museveni Atawazwa Kuwa Askofu wa Kanisa la CNC Uganda

KAMPALA, Uganda — Pastor Patience Rwabwogo, binti wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, ametawazwa kuwa Askofu wa Covenant Nations Church (CNC) katika ibada iliyofanyika Jumapili, Agosti 23, 2026.

Hafla hiyo ilifanyika katika kampasi ya CNC Maya, Wilaya ya Wakiso, na kuhudhuriwa na Rais Museveni pamoja na Mama Janet Museveni, wazazi wa Patience na viongozi wa Uganda.

Miongoni mwa viongozi wengine waliohudhuria ni Makamu wa Rais Jessica Alupo, Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa NRM Moses Kigongo, mawaziri, viongozi wa vyombo vya usalama akiwemo Inspekta Jenerali wa Polisi Abbas Byakagaba, wanadiplomasia na viongozi mbalimbali wa dini.

Ibada hiyo ilifikia kilele muda mfupi baada ya saa 8:00 mchana, ambapo Askofu maarufu kutoka Marekani, Dk. LaDonna Osborn, alimwita Pastor Patience mbele kwa ajili ya kutawazwa rasmi kuwa Askofu.

Katika mahubiri yake akitumia vifungu vya Luka 4:8-21, Osborn alimtaka Askofu Patience kukubali kikamilifu jukumu la kuhubiri Kristo, kulijenga Kanisa na kuendeleza ufalme wa Mungu.

Kabla ya utawazo huo, wazee wa CNC wakiongozwa na Allen Kagina walitoa uthibitisho wa wito na uwezo wa Patience kuongoza kama Askofu.

Patience ndiye mwanzilishi na mchungaji mkuu wa CNC, wakieleza kuwa kanisa hilo lilianza takribani miaka 20 iliyopita kama kikundi kidogo cha waumini kilichokuwa kikikutana nyumbani.

Kwa mujibu wa wazee hao, huduma hiyo imekua kupitia maombi, uvumilivu na mafanikio ya kiroho na sasa imejikita katika mafundisho ya Biblia, uanafunzi, maombi, ibada, uongozi, uinjilisti na huduma kwa jamii.

Viongozi hao pia wamepongeza mchango wa Patience kwa vijana, wakiwemo wanafunzi na wataalamu vijana, kupitia mafundisho ya Biblia, ushauri, mikutano ya uongozi na shughuli za uinjilisti.

Wamesema huduma yake imewahamasisha waumini kutumia elimu, vipaji na fursa walizonazo kwa ajili ya utukufu wa Mungu na manufaa ya jamii.

Kutawazwa kwake kuwa Askofu kunatajwa kuwa hatua muhimu katika safari yake ya zaidi ya miongo miwili ya huduma ya kidini.

Stori na Hasna Thabit | GPL -TUDACO

Leave a Comment