
Dar es Salaam, Agosti 24, 2026 — Mashirika 30 ya Kiraia (CSOs) yanayoongozwa na wasichana na wanawake kutoka Dar es Salaam, Zanzibar na Songwe yamekamilisha mpango wa miezi mitatu wa kujengewa uwezo, huku mashirika 15 yakichaguliwa kupokea ruzuku yenye jumla ya shilingi milioni 375.
Mpango huo umeandaliwa na Foundation for Civil Society (FCS) kwa ushirikiano na UNICEF Tanzania, kwa lengo la kuimarisha uwezo wa mashirika yanayofanya kazi moja kwa moja na jamii katika masuala ya watoto, vijana na wanawake.
Katika kipindi cha Mei hadi Agosti 2026, mashirika hayo yalishiriki mafunzo ya mtandaoni, ushauri elekezi na mafunzo ya ana kwa ana yaliyohusu usimamizi wa miradi, mawasiliano na utetezi, usimamizi wa taasisi, fedha na ruzuku, ulinzi dhidi ya unyanyasaji wa kingono, uhamasishaji wa rasilimali pamoja na uongozi na utawala bora.

Baada ya mafunzo hayo, mashirika yalitakiwa kuwasilisha mapendekezo ya miradi kupitia mchakato wa ushindani.
Mashirika 15 yaliyofanya vizuri katika mchakato huo yamependekezwa kupokea shilingi milioni 25 kila moja, sawa na jumla ya shilingi milioni 375.
Mashirika hayo yanajumuisha matano kutoka Dar es Salaam, matano kutoka Zanzibar na matano kutoka Songwe.
Miradi itakayotekelezwa inalenga maeneo mbalimbali ikiwemo ulinzi wa mtoto, elimu na ujifunzaji mbadala, ustawi wa vijana balehe, usawa wa kijinsia pamoja na kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji na Mkuu wa Ubora wa Programu na Ujifunzaji wa Foundation for Civil Society, Cynthia Bavo, amesema mashirika hayo yana uelewa mkubwa wa changamoto zinazowakabili watoto na vijana katika jamii zao.
Amesema mpango huo umeongeza uwezo wa mashirika hayo katika kutumia maarifa na uzoefu walionao ili kutekeleza miradi yenye matokeo na kuwajibika kwa jamii.
Kwa upande mwingine, wadau wamezitaka taasisi hizo kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha badala ya kutegemea wafadhili pekee.
Wamesema ushirikiano na sekta binafsi, michango ya jamii, kampeni za kuchangisha fedha, taasisi za dini na biashara za kijamii vinaweza kusaidia mashirika kujenga uwezo wa kifedha na kuendelea kutoa huduma kwa jamii.
Mashirika 15 yaliyochaguliwa yanaendelea na mafunzo ya Manage Your Grants kuanzia Agosti 24 hadi 28, 2026, huku utekelezaji wa miradi yao ukitarajiwa kuanza Septemba 1, 2026.