
Yanga SC imeendeleza mwanzo wake mzuri katika msimu mpya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa JKT Tanzania mabao 4-0 katika mchezo uliochezwa jana, Agosti 24, 2026, kwenye Uwanja wa KMC, Mwenge jijini Dar es Salaam.
Yanga ilianza kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya 29 kupitia Albert Kangwanda, aliyefungua ukurasa wa mabao na kuipa timu yake uongozi wa 1-0.
Dakika tano baadaye, Ibrahim Bacca aliifungia Yanga bao la pili dakika ya 34, akimalizia pasi ya Zoukaine na kuongeza presha kwa JKT Tanzania.
Yanga iliendelea kutawala mchezo na juhudi zake zilizaa matunda tena dakika ya 39, ambapo Chadrack Boka alifunga bao la tatu akitumia pasi ya Kangwanda, na kuifanya Yanga kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-0.
Kipindi cha pili, Yanga iliendelea kutawala mchezo huku JKT Tanzania ikishindwa kupata njia ya kurejea mchezoni.

Dakika ya 64, mshambuliaji Peter Shalulile alikamilisha ushindi wa Yanga kwa kufunga bao la nne, akitumia asisti ya Kangwanda na kuifanya timu hiyo kushinda kwa mabao 4-0.
Kangwanda alikuwa miongoni mwa wachezaji walioangaza zaidi katika mchezo huo, akihusika moja kwa moja katika mabao matatu baada ya kufunga bao moja na kutoa asisti mbili. Kiwango hicho kilimfanya atambuliwe kuwa mchezaji bora wa mechi.

Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha ushindi wa tatu katika michezo mitatu ya Ligi Kuu Bara msimu huu. Katika michezo hiyo, mabingwa hao wamefunga jumla ya mabao 11 na kuruhusu mawili pekee.
Matokeo hayo pia yanaifanya Yanga kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi, huku ikiendelea kuweka presha katika mbio za kuwania ubingwa wa msimu wa 2026/27.
Mwanzo huo wa kuvutia unaendelea kuipa Yanga matumaini ya kutetea taji lake, huku safu yake ya ushambuliaji ikionyesha makali katika michezo ya awali ya msimu.
Stori na Na Haika Urio | GPL – TUDACO