×

Airtel Fursa Lab Yazinduliwa Upya, Zaidi ya Watu 5,800 Wanufaika

Dar es Salaam. Wanafunzi, walimu na vijana nchini Tanzania wamepata fursa mpya ya kujifunza na kuendeleza ubunifu wa kiteknolojia baada ya Airtel Africa Foundation kuzindua upya jengo la Airtel Fursa Lab lililopo katika Shule ya Sekondari Kijitonyama, Dar es Salaam.

Airtel Fursa Lab ilianzishwa mwaka 2020 kupitia ushirikiano kati ya Airtel Africa Foundation na Dar Teknohama Business Incubator (DTBi), ikiwa na lengo la kuwawezesha wanafunzi, walimu na vijana kupata ujuzi wa kidijitali, kufanya majaribio na kubuni suluhisho za changamoto zinazowakabili katika maisha ya kila siku.

Tangu kuanzishwa kwake, zaidi ya watu 5,800 wamenufaika na kituo hicho, wakiwemo wanafunzi, walimu, vijana, wajasiriamali na wanawake.

Kituo hicho pia kimekuwa kikitoa fursa kwa wanafunzi waliomaliza Darasa la Saba, Kidato cha Nne na Kidato cha Sita pamoja na wahitimu wa vyuo vikuu kupata ujuzi katika teknolojia, biashara, ubunifu na stadi nyingine za maisha.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa jengo hilo lililokarabatiwa, Mkuu wa Programu kutoka Airtel Africa Foundation, Esi Prah, alisema uwekezaji huo unalenga kuwapa vijana mazingira na zana zinazowawezesha kutumia teknolojia kwa vitendo.

“Tunaamini kuwa upatikanaji wa teknolojia na elimu ya kidijitali unaweza kubadilisha maisha ya vijana kwa kuwapatia maarifa, ujasiri na ujuzi wanaohitaji ili kutengeneza suluhu mbalimbali na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali,” alisema Prah.

Alisema Airtel Fursa Lab imejengwa katika dhana ya kuwapa vijana nafasi ya kujifunza, kufanya majaribio na kugeuza mawazo yao kuwa suluhisho zinazoweza kutumika katika jamii.

Katika kituo hicho, wanafunzi hupata mafunzo na kufanya mazoezi katika maeneo mbalimbali, yakiwemo sayansi ya kompyuta, programu za kompyuta, biashara, stadi za maisha, chakula na lishe pamoja na ushonaji na ubunifu.

Airtel Fursa Lab pia imewaunganisha wanafunzi na majukwaa mbalimbali ya kujifunzia kama ShuleDirect, Maktaba ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na WazoLearn, pamoja na maudhui yanayotumia teknolojia ya akili mnemba (AI).

Kwa miaka kadhaa, kituo hicho kimekuwa sehemu ya kukuza vipaji na ubunifu kwa wanafunzi, huku baadhi ya walionufaika wakifanikiwa kushiriki katika programu mbalimbali na kuwa Mabalozi wa UNICEF na Plan International, wabunifu wa Oky, wasanii wa kidijitali na wabunifu katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM).

Miongoni mwa miradi iliyobuniwa na wanafunzi ni programu ya kufuatilia mzunguko wa hedhi iliyolenga kuwasaidia wasichana kupata taarifa na kufuatilia mizunguko yao.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano, alisema ufunguzi huo mpya unaonyesha dhamira ya kampuni hiyo ya kupanua fursa za elimu ya kidijitali kwa vijana nchini.

“Ukarabati na ufunguzi upya wa Airtel Fursa Lab unaakisi dhamira yetu ya kuhakikisha vijana wa Tanzania wanapata zana, maarifa na fursa wanazohitaji ili kufanikiwa katika dunia ya kidijitali,” alisema Singano.

Alisema lengo ni kuhakikisha teknolojia inatumika kama nyenzo ya elimu, ubunifu na kujenga fursa za kiuchumi, badala ya kubaki kuwa chombo cha mawasiliano pekee.

“Kupitia ushirikiano wetu, Airtel sasa imeunga mkono zaidi ya shule tano, na tutaendelea kufanya kazi na washirika wetu kuwafikia vijana na jamii nyingi zaidi,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kijitonyama, Halima Juma, alisema Airtel Fursa Lab imekuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya shule hiyo katika TEHAMA na ubunifu.

“Tangu mwaka 2020, Fursa Lab imewawezesha wanafunzi na walimu wetu kupata ujuzi wa kidijitali, mafunzo ya vitendo na fursa za ubunifu,” alisema Juma.

Alisema kituo hicho kimepanua wigo wa shule kwa kuwapa vijana kutoka nje ya shule hiyo nafasi ya kupata maarifa na ujuzi wa kidijitali.

Matokeo ya uwekezaji huo yanaonekana pia katika mafanikio ya Shule ya Sekondari Kijitonyama, ambayo imeorodheshwa katika nafasi ya 10 kitaifa katika TEHAMA kwa miaka mitatu mfululizo.

Aidha, wanafunzi wa shule hiyo wameshinda tuzo tatu katika mashindano ya Girls in ICT, yanayolenga kuhamasisha ushiriki wa wasichana katika teknolojia.

Miongoni mwa wanafunzi walionufaika na Fursa Lab ni Angel Swai, ambaye amebuni suluhisho la taa za kuongozea magari linalotumia akili mnemba (AI).

Angel alisema Fursa Lab imemsaidia kwenda zaidi ya nadharia anayojifunza darasani na kupata nafasi ya kufanya majaribio ya mawazo yake.

“Airtel Fursa Lab imenipa nafasi ya kujifunza, kufanya majaribio na kubadilisha mawazo yangu kuwa kitu cha vitendo,” alisema.

Alisema mazingira na rasilimali zinazopatikana katika kituo hicho zimemsaidia kuelewa namna teknolojia na AI zinavyoweza kutumika kutatua changamoto halisi katika jamii.

“Ubunifu wangu ni mfano wa kile ambacho vijana wanaweza kufanikisha wanapopewa zana na fursa zinazofaa,” alisema.

Ukarabati wa Airtel Fursa Lab unatarajiwa kuendelea kutoa nafasi kwa wanafunzi, walimu na vijana wengine kujifunza ujuzi wa kidijitali, kufanya majaribio na kukuza ubunifu.

Shule ya Sekondari Kijitonyama imeishukuru Airtel Africa Foundation, Airtel Money, DTBi na Serikali ya Tanzania kwa kuunga mkono mpango huo na kuongeza fursa za elimu ya kidijitali kwa wanafunzi, walimu na jamii kwa ujumla.

Leave a Comment