×

Ayra Starr Aandika Historia Billboard, “Starrgirl” Yaingia Namba 4 Duniani

Mwimbaji wa Nigeria, Ayra Starr, ameendelea kuonyesha nguvu ya muziki wa Afrika katika soko la kimataifa baada ya album yake mpya “Starrgirl” kuingia katika nafasi ya nne kwenye Billboard World Albums Chart.

Mafanikio hayo yanaifanya “Starrgirl” kuwa miongoni mwa miradi iliyofanya vizuri kwenye chati hiyo, huku Ayra Starr akiendelea kujenga jina lake katika soko la muziki duniani.

Hii ni mara ya kwanza kwa Ayra Starr kuingia kwenye Billboard World Albums Chart kupitia album yake kama msanii wa solo, hatua inayochukuliwa kuwa moja ya mafanikio makubwa katika safari yake ya muziki pamoja na kuongeza heshima kwa muziki wa Nigeria.

Album hiyo ilitolewa rasmi Agosti 14, 2026, kupitia Mavin Records na Republic Records, ikiwa ni album yake ya tatu ya studio.

“Starrgirl” inafuatia album zake mbili zilizotangulia, “19 & Dangerous” iliyotoka mwaka 2021 na “The Year I Turned 21” iliyotolewa mwaka 2024.

Album hiyo ina jumla ya nyimbo 16, huku Ayra Starr akiwashirikisha baadhi ya majina makubwa kutoka Nigeria na kimataifa, akiwemo Wizkid, Rema, ZAYN, Leon Thomas, kwn, Theodora na Danny Ocean.

Miongoni mwa nyimbo zinazopatikana kwenye album hiyo ni “Gimme Dat” akiwa na Wizkid, “Who’s Dat Girl” akiwa na Rema na “Heaven Baby” akiwa na ZAYN.

“Starrgirl” Yawa Mbele ya Album ya Tyla

Katika Billboard World Albums Chart, “Starrgirl” imeingia katika nafasi ya nne, ikiwa nyuma ya miradi mitatu ya K-pop.

Nafasi ya tano imechukuliwa na album “APOP” ya msanii wa Afrika Kusini, Tyla, hivyo Ayra Starr ameweka “Starrgirl” mbele ya album hiyo katika chati.

Mafanikio hayo yamekuja ndani ya muda mfupi tangu album hiyo itoke, jambo linaloendelea kuongeza uzito wa Ayra Starr katika muziki wa Afrobeats na soko la muziki la kimataifa.

Kwa kuingia katika nafasi ya nne kwenye Billboard, Ayra Starr anaendelea kuthibitisha kuwa wasanii wa Afrika wana uwezo wa kushindana katika majukwaa makubwa ya muziki duniani na kuvuka mipaka ya bara hilo.

Stori na Razaku Ramadhan | GPL – TUDACO

Leave a Comment