
Klabu ya Barcelona imekamilisha usajili wa kipa wa kimataifa wa Croatia, Dominik Livaković, kutoka Fenerbahçe kwa mkataba wa miaka minne utakaomuweka klabuni hapo hadi Juni 2030.
Livaković, mwenye umri wa miaka 31, amejiunga na Barcelona kwa ada ya awali ya Euro milioni 2, huku thamani ya uhamisho huo ikitarajiwa kufikia hadi Euro milioni 4 iwapo bonasi zilizowekwa kwenye makubaliano zitatimia.
Kipa huyo anaingia Barcelona akiwa na uzoefu mkubwa wa kimataifa, baada ya kutumia misimu miwili akiwa na Fenerbahçe, ambapo alicheza mechi 74 na kuweka clean sheet 24.
Mbali na uzoefu wake katika ngazi ya klabu, Livaković amekuwa sehemu muhimu ya timu ya taifa ya Croatia, akiichezea nchi hiyo katika Kombe la Dunia mara tatu pamoja na michuano miwili ya UEFA Euro.
Usajili wake unafanyika wakati Barcelona ikiendelea kufanya maboresho katika nafasi ya golini, kufuatia Marc-André ter Stegen kuondoka kwa mkopo kwenda Ajax.
Kuwasili kwa Livaković kunatarajiwa kuongeza ushindani katika nafasi ya kipa, huku Barcelona ikitarajia kutumia uzoefu wake katika mashindano ya ndani na ya kimataifa.
Kwa upande wa Livaković, uhamisho huo unampa nafasi ya kuanza ukurasa mpya katika soka la juu la Ulaya akiwa sehemu ya moja ya klabu kubwa zaidi duniani.
Stori na Haika Urio | GPL-TUDACO