×

Rais wa Iran Akiri Vikwazo vya Marekani Vinaumiza Uchumi

TEHRAN, Iran: Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amekiri kuwa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani vinaendelea kuathiri uchumi wa nchi hiyo, siku chache baada ya kusema kuwa hatua hizo hazitakuwa na mafanikio.

Akizungumza na televisheni ya taifa ya Iran Ijumaa usiku, Pezeshkian amesema baadhi ya watu wamekuwa wakidai kuwa vikwazo hivyo havina madhara yoyote, lakini hali halisi ni tofauti.

“Wengine wanasema vikwazo havina athari kabisa; kwa watu hao, kwa kweli sijui niseme nini,” Pezeshkian amesema.

Amesema Iran kwa sasa iko katika hali ya vita na hivyo wananchi wanapaswa kukubaliana na mazingira magumu yanayoikabili nchi hiyo.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent, kutangaza mipango ya kuongeza shinikizo la kiuchumi dhidi ya Iran, akionya nchi zitakazokataa kushiriki katika kampeni hiyo.

Hatua hizo mpya zinaendeleza vikwazo vilivyowekwa na Marekani na washirika wake tangu mwaka 2018, baada ya Rais Donald Trump wa wakati huo kuiondoa Marekani katika makubaliano ya kimataifa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Pezeshkian amesema katika miezi ya hivi karibuni, kiwango cha bidhaa zinazoingia na kutoka nchini Iran zimepungua kwa asilimia 25 hadi 35, akidai hali hiyo inatokana pia na zuio la majini la Marekani katika bandari za Iran.

Kutokana na kupungua kwa biashara, Rais huyo amesema kuna haja ya kuongeza bei ya mafuta ya petroli nchini Iran ili kukabiliana na hali hiyo.

Ameeleza kuwa bei ya moja ya viwango vya matumizi ya mafuta inaweza kuongezwa kutoka tomani 5,000 hadi tomani 10,000.

Iran ni miongoni mwa nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani na imekuwa ikitoa ruzuku kubwa kwa mafuta ya petroli, jambo linalofanya suala la kuongeza bei kuwa nyeti kisiasa.

Hata hivyo, siku hiyo hiyo Pezeshkian alisisitiza kuwa vikwazo vipya vya Marekani “havitatimiza chochote,” akisema Iran itaendelea kukabiliana na shinikizo la kiuchumi.

Kauli zake za hivi karibuni zinaashiria mabadiliko ya msimamo kuhusu ukubwa wa athari za vikwazo hivyo, huku serikali ya Iran ikikabiliwa na changamoto za biashara, uagizaji wa mafuta na hali ya uchumi wa ndani.

Leave a Comment